Na Marco Maduhu & Kadama Malunde - Shinyanga
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imewataka Majaji, Mahakimu na Mawakili kutokuwa chanzo cha migogoro ndani ya jamii kutokana na baadhi yao kudaiwa kutotoa maamuzi yasiyo ya haki kwenye migogoro wanayoisikiliza.
Rai hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika Februari 3, 2025, katika viwanja vya mahakama hiyo.
Jaji Mahimbali amesisitiza kuwa taasisi za haki, hasa Mahakama, zinatakiwa kuwa suluhisho la migogoro na siyo chanzo cha migogoro zaidi.
Ametoa wito kwa Majaji, Mahakimu na Mawakili kuwa makini na kutoa maamuzi yenye haki ili kuongeza imani ya wananchi kwa mfumo wa sheria.
"Maamuzi yetu lazima yatoe suluhisho, siyo kuchochea migogoro zaidi. Tunatakiwa tutatue migogoro badala ya kuwa chanzo cha migogoro, tunataka wananchi warudishe Imani kwetu kwa kuhakikisha tunawapa huduma bora kwa wakati. Maamuzi yetu yatoe suluhisho la migogoro na matatizo yaliyofikishwa mahakamani”,amesema Jaji Mahimbali.
Maadhimisho hayo yametanguliwa na Wiki ya Sheria iliyofanyika Januari 25,2025 hadi Februari 1,2025, ambapo Mahakama Kuu ya Shinyanga ilitekeleza mkakati wa kutoa elimu ya sheria kwa wananchi katika maeneo yao, ili kuimarisha ufahamu wa sheria na haki.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ilikuwa "Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai Katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo."
Jaji Mahimbali ameeleza kuwa maboresho ya Mahakama ni muhimu katika kufikia malengo ya uchumi wa kati na maendeleo ifikapo 2050.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa wananchi kufuatilia kesi zao mahakamani na kuepuka kusababisha kesi kufutwa kwa kutohudhuria, huku akionya dhidi ya kujichukulia sheria mikononi mwao.
“Ni muhimu wananchi mfike mahakamani ili kuepuka kesi kufutwa, huku mahakamani hatufugi kesi, usipohudhuria mahakamani sisi tunafuta kesi”,amesema.
Mahakama imejipanga kutekeleza malengo ya taifa ya maendeleo, na Jaji Mahimbali amehimiza taasisi za haki za madai kujipanga kuhakikisha kuwa mfumo wa haki unakua na kudumu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Wakili Julius Mtatiro amesema Serikali ya mkoa wa Shinyanga inaridhishwa na mahakama kama mhimili wa dola wenye kufanya kazi katika kujenga ustawi wa mkoa.
"Mahakama ya leo siyo kama zamani ambapo kumfikia Hakimu au Jaji ilikuwa vigumu, leo kuna mabadiliko ya kimfumo ya uendeshaji shughuli za mahakama, na Majaji wa wanafikika na kwamba wajibu wa Mahakama ni kumfikia mwananchi na kutenda haki",amesema.
"Leo Jaji anakutana na mteja na kumuelekeza zamani ilikuwa vigumu,kwanza kumsogelea tu Jaji unahukumiwa,"ameongeza Mtatiro.
Aidha,ameiomba Mahakama iendelee kuwa ukaribu na Wananchi na kutoa elimu ya sheria ili wajue kudai haki zao kwa mujibu wa sheria.
"Tunahitaji kujenga Taifa la wananchi lenye kujua haki zao kisheria, na hata kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhoji, hii itasaidia pia kujenga uwajibikaji kwa viongozi," amesema Mtatiro.
Ametaja pia baadhi ya changamoto kwamba kumekuwepo na tatizo la wananchi wa kipato cha chini kushindwa kupata haki zao kisheria sababu ya kukose pesa za kuwalipa Mawakili,huku akiomba mfumo wa haki uendelee kuimarishwa zaidi ili wananchi waendelee kuwa na imani na Mahakama.