![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh6xoo6VH5Ze8rFmjpmHci0g3Nnh3Z1adi6Yd12MlZUxWaveNd0KCMv2vbW4NEj2W6DdDFHksrQqjuDyIqVTSFiJPMe44hWZkxf7zu3lT-QMoAoWGZ8sh0tg73fPbRXVGFltVNHU0IKbXfYgVT-BLmkiS_6vtxy7AkEnlQKjzEUfoMx-yCI0KlPjoTcZw/s600/DSC_3283.jpg)
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali
Na Marco Maduhu & Kadama Malunde, Shinyanga
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, imefanya kikao cha wadau kutathmini maadhimisho ya Wiki ya Sheria 2025, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga.
Kikao hicho kimefanyika leo Februari 6, 2025, kikihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Mahakama ambapo kililenga kujadili mafanikio na changamoto za maadhimisho ya mwaka huu pamoja kujipanga kwa ajili ya maadhimisho yajayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali, amewashukuru wadau wa Mahakama kwa kufanikisha maadhimisho hayo kwa kiwango kikubwa, huku akiahidi kufanyia kazi ushauri wao ili kuboresha maadhimisho ya mwaka ujao.
"Nawashukuru wadau wa Mahakama kwa kufanikisha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria 2025, hivyo tumekutana hapa kwa ajili ya kikao cha tathmini, ili kupata maoni, changamoto, na kujadili namna ya kuboresha zaidi katika maadhimisho yajayo",amesema Jaji Mahimbali.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bakari Mketo, amesisitiza umuhimu wa wadau katika kufanikisha maadhimisho ya Wiki ya Sheria, na kuwashukuru kwa michango yao.
"Wadau wa Mahakama ni wa muhimu sana katika kufanikisha maadhimisho haya, na kwa hiyo tunawashukuru kwa kutushika mkono",amesema
Kikao hicho cha tathmini pia kimehusisha utoaji wa vyeti vya shukrani na pongezi kwa wadau wa Mahakama, wakiwemo waandishi wa habari, ambao wamechangia katika kufanikisha maadhimisho hayo.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ilizindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria Januari 25, 2025, katika Viwanja vya Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga, na kuhitimisha Februari 3, 2025, katika Viwanja vya Mahakama Kuu.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa, "Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo."
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEga7_jph98-DJ75BNjmcb6yNF4kYQnj48FuQiHJwwVskdM777siUrHt666IrKJSdViwq7f9gkdhCLHh5rL68EcEwzpdlN5DizNj1AewHBeo9PEHzw4fS1HYEKTbtsoPh9wx0NLzn0iJiElRJ1a851NLdBAp2UXia5bLgifeWmNn-SstLr3_Y_SF8bAMlA/s600/DSC_3298.jpg)