TAKUKURU YAOKOA MILIONI 137.8 FEDHA ZA MAUZO YA VIWANJA KAHAMA

TAKUKURU YAOKOA MILIONI 137.8 FEDHA ZA MAUZO YA VIWANJA KAHAMA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU)Mkoa wa Shinyanga,imeokoa kiasi cha fedha sh.milioni 137.8 za mauzo ya viwanja katika Manispaa ya Kahama,kutokana na baadhi ya watu waliomilikishwa viwanja hivyo kutolipa gharama halisi ya mauzo ya viwanja.
Hayo yalibainishwa leo Februari 4,2025 na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kwa kipindi cha robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Disemba 2024/2025

Amesema kwa kipindi hicho wamefanikiwa kuokoa sh.milioni 137.8 ikiwa ni sehemu ya fedha za mauzo vya viwanja 29 vilivyopimwa na Manispaa ya Kahama mwaka 2019, na kwamba katika viwanja hivyo ilitolewa gharama halisi ambayo wananchi wangepaswa kulipa, lakini viwanja vitatu (3) ndiyo vililipwa fedha halisi,huku 26 malipo yakiwa siyo sahihi.
“Manispaa ya Kahama ilikuwa ikimiliki ardhi katika maeneo ya kimkakati eneo la Phantom, na mnamo mwaka 2019 ili amua kupima eneo hilo na kuuza viwanja kwa mtu yoyote anayehitaji, na vilipatikana viwanja 29 ambavyo vilipaswa kumilikishwa kwa wananchi kwa gharama ya sh. 15,000 kwa mita moja ya mraba, na viwanja vya biashara sh.20,000,”amesema Kessy.

“Mwaka 2024 Takukuru kupitia vyanzo vyetu vya siri, tulipata taarifa kwamba, baadhi ya wananchi wamemilikishwa viwanja hivyo bila ya kulipa gharama zilizohitajika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Manispaa ya Kahama,tulibaini kuwa kati ya viwanja 29 ni viwanja vitatu pekee wamiliki wake walilipa malipo halali, lakini 26 havikulipwa kwa gharama halisi,vyenye thamani ya sh.milioni 800,”ameongeza.
Amesema baada ya kubaini hilo, waliweza kuwafikia wamiliki wa viwanja hivyo 26, na kuwataka walipe gharama halisi ya mauzo ya viwanja hivyo au vitangazwe upya,na walikubali kufanya malipo kama walivyopaswa,na kwamba sh.milioni 137.8 zimeshalipwa kati ya sh.milioni 800,huku wakiendelea pia kufuatilia fedha zingine zilizobaki sh.milioni 662.2,ili kuhakikisha viwanja vyote vinalipiwa na fedha zake kuingizwa serikalini.

Aidha,amesema kwa upande wa dawati la uchunguzi walipokea malalamiko 38,yaliyohusu rushwa ni 20 yasiyo husu rushwa ni 18, na kwamba uchunguzi wake unaendelea, huku akibainisha kuwa wamejipanga pia kuzuia vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwaka huu 2025.

Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, kwamba waendelee kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vyovyote vya vitendo vya rushwa,ikiwa pamoja na miradi ya maendeleo ili hatua za haraka zichukuliwe.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464