MADIWANI MANISPAA YA SHINYANGA WAJADILI TAARIFA MBALIMBALI KIKAO CHA BARAZA,WAULIZA MASWALI YA PAPO KWA PAPO KWA MAENDELEO YA WANANCHI
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wamejadili taarifa mbalimbali kwenye kikao cha baraza cha robo ya pili,kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya wananchi na Halmashauri hiyo.
Kikao hicho cha baraza la Madiwani kimefanyika leo Februari 6,2025 katika ukumbi wa mkutano wa halmashauri hiyo pamoja na kuhudhuriwa na wananchi.
Mmoja wa Madiwani hao Victor Mkwizu wa Ngokolo,aliuliza swali la papo kwa papo,kwamba ujenzi wa kituo cha polisi katika Majengo Mapya umechukua muda mrefu kushindwa kukamilika zaidi ya miaka mitano kuwa ni lini ujenzi huo utakamilishwa.
Diwani wa Ndembezi Victor Mmanywa,naye aliuliza swali juu ya kusua kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Ndembezi, kwamba utakamilishwa lini na ulianzishwa kwa nguvu za wananchi zaidi ya miaka mitano.
Diwani mwingine wa Vitimaalumu Pica Chogelo, naye aliuliza swali juu ya upimaji wa viwanja katika Kata ya Mwamalili.
Enock Lyeta diwani wa Oldshinyanga,aliuliza swali la wananchi 9 kuwa watalipwa lini fidia zao katika eneo la Butulwa.
Diwani wa Mwawaza Juma Nkwambi naye aliuliza swali juu ya hatua za ujenzi wa Stendi ya Mabasi Mwawaza.
Akijibu maswali hayo Mchumi wa Manispaa ya Shinyanga Mensaria Mrema,amesema kwa upande wa maboma yote ambayo yalianzishwa kwa nguvu za wananchi pamoja na Halmashauri, kwamba taarifa zake zimepelekwa TAMISEMI ili yaweze kupewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Afisa Ardhi Jacob Mwinuka,akijibu swali la upimaji viwanja eneo la Mwamalili, amesema kwamba upimaji wa eneo husika inategemea na uhitaji wa wananchi,na kutoa ufafanuzi kwamba wananchi kupitia kwenye kamati zao za maendeleo ya Kata kuwa wajadili na kuomba kupimiwa maeneo yao.
Kwa upande wa ulipwaji fidia wananchi katika eneo la Butulwa Oldshinyanga, amesema kwamba tayari fedha zimeshatengwa kwenye bajeti ijayo na kwamba watalipwa fidia zao.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko,amesema Manispaa hiyo itajitahidi kukamilisha maboma ambayo yameanzishwa kujengwa kwa nguvu za wananchi,moja baada ya jingine kupitia fedha za mapato ya ndani.
Amewaagiza pia Maafisa Watendaji wa Kata,kwamba wanapokuwa wakiandaa taarifa za Kata kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ili kupitishwa,wawe makini na uandaaji wa taarifa hizo na kusiwepo na mapungufu.
Pia,amemuagiza Mkurungenzi wa Manispaa ya Shinyanga,kuchukua hatua ya kuwaondoa watu ambao wanaishi kwenye eneo la shule ya msingi Lubaga na wameweka na zizi la Ng'ombe.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Revocatus Lutunda,amewapongeza Madiwani hao kwa ushiriki mzuri wa kikao hicho cha baraza, na kuhoji mambo mbalimbali kwa ajili ya mustakabaki wa maendeleo ya wananchi.
Aidha,amesema kwa maelekezo ambayo yametolewa kwenye kikao hicho, Menejment imeyachukua na itayafanyia kazi.
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga,amesema baraza hilo la Madiwani Manispaa ya Shinyang, kwamba lipo makini na linaendeshwa kwa weledi mkubwa.
TAZAMA PICHA 👇👇
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Revocatus Lutunda akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Baraza la madiwani likiendelea.