MANISPAA YA SHINYANGA YAJIPANGA KUIMARISHA HALI YA USAFI ZAIDI KUUWEKA MJI KATIKA MAZINGIRA MAZURI

MANISPAA YA SHINYANGA YAJIPANGA KUIMARISHA HALI YA USAFI ZAIDI KUUWEKA MJI KATIKA MAZINGIRA MAZURI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga, imejipanga kuendelea kuimarisha hali ya usafi wa mazingira, ili kulinda tuzo ya usafi ambayo ilishinda kutoka Wizara ya Afya pamoja na kuweka Mji katika mazingira mazuri.

Hayo yamebainishwa leo Februari 7,2025 kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani cha Robo ya Pili, wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Kamati ya Mipango Miji na Mazingira.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Revocatus Lutunda, amebainisha hayo wakati akijibu swali aliloulizwa na Diwani wa Kizumbi Rubeni Kitinya,juu ya uimarishaji wa usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo.

Amesema ili kuendelea kulinda hadhi ya Manispaa hiyo kuwa mji msafi na kulinda tuzo ya usafi wa mazingira kutoka wizara ya afya, kwamba wameweka mikakati madhubuti ya kuendelea kuimarisha hali ya usafi zaidi, pamoja na kukumbusha wananchi kufanya usafi katika maeneo yao.
“Suala la usafi kwa kweli katika mji wetu tumelegalega hali siyo nzuri, lakini tumeweka mikakati ya kuimarisha usafi zaidi,kukumbusha wananchi kufanya usafi, pamoja na kutenga siku maalumu ya kuwa tunafanya usafi, ili kuendelea kulinda heshima ya tuzo yetu ya usafi wa mazingira,”amesema Lutunda.

Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko, naye amesisitiza suala la usafi kwenye mji huo, na kwamba uchafu kwa sasa umeanza kuonekana, ili kuendelea kulinda heshima yao ya kupata tuzo ya ushindi wa usafi wa mazingira ngazi ya miji.
Awali Diwani wa Kizumbi Rubeni Kitinya, aliuliza swali juu ya mikakati ambayo manispaa ya Shinyanga imechukua, dhidi ya kuimarisha hali ya usafi wa mazingira, ambapo kwa sasa hali imeanza kuwa siyo nzuri kutokana na maeneo mengi kuwa machafu.

Amewalalamikia pia Mawakala wa kukusanya uchafu,kuwa wameshindwa kufanya kazi zao vizuri, huku wakati wa uzoaji wa Taka kwenye Magari yao kupeleka dampo, kwamba wamekuwa wakiagusha uchafu hovyo barabarani na kusababisha mji kuonekana kuwa mchafu.

TAZAMA PICHA👇👇
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza kwenye kikao cha Baraza.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Revocatus Lutunda akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Kikao cha Baraza la Madiwani kikiendelea.
Diwani wa Kizumbi Rubeni Kitinya akiuliza swali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Baraza la Madiwani likiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464