RC MACHA AWAITA WANANCHI WAJITOKEZE KUPIMA UGONJWA WA KIFUA KIKUU,MATIBABU YANATOLEWA BURE
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo,wajitokeze kwa wingi kupima ugonjwa wa kifua kikuu, ambapo tiba yake itatolewa bure.
Amebainisha hayo leo Februari 8,2025 wakati akizindua Kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wenye vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu.
Amesema kupitia kampeni hiyo, amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima ugonjwa wa kifua kikuu, na watakaobainika kuwa na ugonjwa huo waanze kupata matibabu ambayo hutolewa bure kuanzia vipimo hadi madawa.
“Mkoa huu wa Shinyanga watu wenye tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu wapo 2,903 huku watu 1,349 bado hawajafikiwa,ambao ndiyo wanatafutwa kupitia kampeni hii, na ugonjwa huu ni hatari una ambukizwa kwa njia ya hewa,”amesema Macha.
Amesema kwamba mtu mmoja mwenye tatizo la kifua kikuu, kwa mwaka mmoja anaweza kumbukiza watu 20, na kwamba hatua zisipochukuliwa mapema tatizo litakuwa kubwa, na ndiyo maana serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inaendesha kampeni hiyo ili kuokoa afya za wananchi.
Aidha, amewataka wananchi kwamba wanapotumia dawa za kifua kikuu wamalize dozi, na siyo kukatisha hali ambayo inasababisha ugonjwa kuwa usugu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John,amesema kwa takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2023,kwamba watu milioni 10.8 waligundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu, na milioni 2.5 walifariki dunia.
Amesema ugonjwa wa kifua kikuu asilimia 45 unaathiri sana nchi za Asia na 24 nchi za Afrika, na kwamba tafiti zinaonyesha kati ya watu 100, watu 25 wana tatizo la kifua kikuu.
Ametaja dalili za ugonjwa wa kifua kikuu, kuwa ni kukohoa muda wote, homa za muda mrefu,mwili kupungua uzito, kutokwa jasho hasa nyakati za usiku,na huambukizwa kwa njia ya mfumo wa hewa.
Dk.Luzila ametaja aina za TB, kuwa kuna Tb ya Moyo,Mifupa ya Mgongo, Ubongo, na Tb ya Mapafu,
“Takwimu za mwezi januari ambazo tulipima watu 84, watu 6 waligundulika kuwa na vimelea vya kifua kikuu, na mwezi februari tulipima pia watu 28 na watu 3 walikuwa na vimelea kifua kikuu na walianza kupata matibabu,”amesema Dk.Luzila.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile, amesema kampeni hiyo harakishi ni kuibua wagonjwa wa kifua kikuu ambao hawajafikiwa, na lengo ni kufikia watu 1,349 ili wapate tiba na wasiambukize tena.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salumu Hamduni amesema kampeni hiyo ni endelevu,na huduma zake ni bure na inaratibiwa na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na wadau wa kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu.
Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga akiwamo Magera Seni,ambaye amejitokeza kupima vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu, ameishukuru serikali kwa kampeni hiyo, ambayo imelenga kuokoa afya za wananchi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salumu Hamduni akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Uzinduzi wa kampeni ya harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu ukiendelea.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464