RC MACHA AKEMEA IMANI POTOFU MATUMIZI YA VYANDARUA VYA SERIKALI KUKABILIANA NA UGONJWA WA MALARIA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuendekeza imani potofu juu ya matumizi ya vyandarua ambavyo vinatolewa na serikali ili kukabiliana na ugonjwa wa Malaria, na hata kuvitumia kwa matumizi yasiyokusudiwa ikiwamo kuvulia samaki, kuzungushia bustani,na kufugia kuku.
Amebainisha hayo leo Februari 8,2025 wakati akizundua kampeni ya ugawaji vyandarua ngazi ya Kaya, mara baada ya kumalizika kwa zoezi la uandikishaji, hafla iliyofanyika katika Zahanati ya Olshinyanga, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na chama.
Amesema kwa mwananchi ambaye ataendekeza imani potofu na kutumia vyandarua ambavyo vimetolewa na serikali bure, kwa matumizi ambayo siyo sahihi, atachukuliwa hatua kali pamoja na kurudisha fedha ya chandarua alichopewa.
“Watendaji wa Vijiji,Vitongoji na Mitaa,msione haya kuwachukulia hatua watu ambao watatumia vyandarua hivi vya serikali kwa matumizi yasiyo sahihi, na sisi pia tutafanya ufuatiliaji kaya kwa kaya,”amesema Macha.
“Vyandarua hivi ni salama vinadawa ya kuulia Mbu, na havihusiana na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume, wala kugunguni, vitumieni ili mjikinge na ugonjwa wa Malaria,”ameongeza Macha.
Amewasihi pia wananchi, kwamba katika kukabiliana na ugonjwa huo wa Malaria, wafanye usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuondoa mazalia ya Mbu, na kwamba pale wanapo hisi wameambukizwa ugonjwa huo wakapime na kupata matibabu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk,Yudas Ndungile ametaja takwimu za kiwango cha Maambukizi ya ugonjwa wa Malaria mkoani humo kwamba ni asilimia 16, huku kitaifa ni asilimia 8.1 na Mkoa huo upo nafasi ya 4 kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya,Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria Peter Gitanya, naye amesisitiza wananchi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vya serikali, na kwamba waachane na imani potofu ili ifikapo 2030 kusiwepo na ugonjwa wa Malaria hapa nchini.
Mkurugenzi wa Ugavi na uendeshaji kutoka Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) Victor Sungusia, ambao ndiyo wasambazaji wa vyandarua hivyo, amesema katika Mkoa wa Shinyanga kuna Vituo 600, na watasambaza vyandarua kwa wananchi milioni 1.5 kwa wale ambao walijiandikisha, na zoezi hilo litachukua muda wa siku 10.
Nao baadhi ya wananchi ambao wamepewa vyandarua hivyo, wameipongeza serikali kwa kuendelea kujali afya zao, na kuahidi kuvitumia ili kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza wakati wa uzinduzi kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya serikali vyenye dawa ngazi ya Kaya.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza wakati wa uzinduzi kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya serikali vyenye dawa ngazi ya Kaya.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Anord Makombe akizungumza wakati wa uzinduzi kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya serikali vyenye dawa ngazi ya Kaya.
Mkurugenzi wa ugavi na uendeshaji kutoka MSD Victor Sungusia akizungumza wakati wa uzinduzi kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya serikali vyenye dawa ngazi ya Kaya mkoani Shinyanga.
Mwakilishi kutoka TAMISEMI Best Yoram akizungumza wakati wa uzinduzi kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya serikali vyenye dawa ngazi ya Kaya mkoani Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza wakati wa uzinduzi kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya serikali vyenye dawa ngazi ya Kaya.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Peter Gitanya akizungumza wakati wa uzinduzi kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya serikali vyenye dawa ngazi ya Kaya mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akigawa vyandarua vya serikali vyenye dawa kwa wananchi ambao walijiandikisha kupata vyandarua hivyo ili kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.
Katibu Tawala wa wilaya ya ya Shinyanga Said Kitinga akisherehesha kwenye hafla hiyo ya ugawaji wa vyandarua kwa wananchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464