MKUTANO WA KITAIFA WA AFYA YA AKILI KUFANYIKA SHINYANGA
MKUTANO wa Kitaifa wa Afya ya Akili,unatarajiwa kufanyika mkoani Shinyanga katika wilaya ya Kahama, kwa kukutanisha watu mbalimbali wakiwamo wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo Februari 21,2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa Mkutano huo wa Kitaifa wa Afya Akili Faustine Mlyutu,wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema Mkutano huo wa Kitaifa wa Afya ya Akili,utafanyika May 30-31 mwaka huu, ambao utakutanisha watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, ili kujadili kwa pamoja namna kutatua tatizo hilo la Afya ya Akili.
“Malengo yetu ni kukutanisha watu 500 kutoka ndani na nje ya nchi, kutambua madhara yatokanayo na Afya ya Akili, na kujadili juu ya utatuzi wa tatizo hili, sababu limekuwa janga kubwa la kitaifa,”amesema Mlyutu.
Meneja Mpango Magonjwa yasiyoambukiza Edith Bakari kutoka Wizara ya Afya, amesema faida ya mkutano huo ni serikali kujadili na wadau, ili kuja na mpango wa pamoja kuona namna ya kutatua tatizo la Afya ya Akili ndani ya jamii.
Naye Christiani Alais kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Milembe Jijini Dodoma, amesema tatizo la Afya ya Akili ni kubwa hapa nchini, na kwamba katika hospitali hiyo kila mwaka hupokea wagonjwa elfu 50.
Mkurugenzi wa Shirika la WAYDS Charles Deogratius, ambao ndiyo waandaaji wa Mkutano huo wa Kitaifa wa Afya ya Akili,amesema tatizo la Afya ya Akili ni ugonjwa kama mwingine, hivyo watu wenye shida hiyo hawapaswi kunyanyapaliwa, bali ni kusaidiwa ili wapate huduma ya matibabu, na wasiwawekee Imani potofu kuwa wamerogwa.

TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa Maandalizi wa Mkutano wa Kitaifa wa Afya ya Akili Faustine Mlyutu akizungumza na waandishi wa habari.
Meneja Mpango Magonjwa yasiyoambukiza Edith Bakari kutoka Wizara ya Afya akizungumza na waandishi wa habari.
Christiani Alais kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Milembe Jijini Dodoma,akizungumza na waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Shirika la WAYDS Charles Deogratius, akizungumza na waandishi wa habari.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Maandalizi ya Mkutano wa Kitaifa wa Afya ya Akili ambao utafanyika Mkoani Shinyanga katika wilaya ya Kahama.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464