RAS CP. HAMDUNI AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA

RAS CP. HAMDUNI AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni,amezindua bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, na kueleza kwamba bodi hiyo ni ya muhimu katika uendeshaji wa huduma za afya na kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi.
Bodi hiyo imezinduliwa leo Februari 11,2025.

CP. Salum akizundua Bodi hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amewapongeza Wajumbe kwa kuteuliwa na Waziri wa Afya Mwenye dhamana kuisimamia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga,na kwamba kazi ya Bodi ni kuishauri Menejimenti ya Hospitali katika utendaji wake kazi ili kuboresha huduma za afya.
“Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ni chombo muhimu sana katika uendeshaji wa huduma za afya za Hospitali. na ni kiungo kinachowaunganisha wananchi na serikali yao ngazi ya Hospitali ya Rufaa na kuboresha utoaji wa huduma,”amesema CP Hamduni.

“kazi kubwa ya Bodi ni kuisimamia kwa ukaribu sana Menejimenti ya Hospitali katika utekelezaji wa majukumu yake, kimsingi Menejmenti ya hospitali inawajibika moja kwa moja kwa bodi,hivyo wajumbe tumieni taaluma zenu kuisaidia hospitali katika uendeshaji wa huduma za afya,”ameongeza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile. Amesema Bodi hiyo ni wawakilishi wa watumiaji wa huduma ambayo inatolewa hospitali, na kwamba wakisikia kuna malalamiko au manun’guniko juu ya utoaji wa huduma katika hospitali hiyo, basi wawasiliane na Menejimenti ili yapate kutatuliwa.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dk.Fadhili Kibaya,amesema Bodi hiyo itadumu kwa muda wa miaka mitatu, na kwamba kazi yake ni kuhakikisha hospitali inatoa huduma bora za matibabu kwa wananchi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John, amesema hospitali hiyo ilianzishwa Rasmi mwaka 1947 ikiwa kama Kituo cha kutolea huduma baada ya Vita ya kuu ya pili ya dunia, ambapo ilijengwa kwa nguvu za wananchi.

Amesema mwaka 1974 ilipanda daraja kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na mwaka 2010 ikatangazwa Rasmi, na kwamba mwaka 2014 ilianza kujengwa Hospitali mpya Kata ya Mwawaza, na huduma za matibabu zilianza kutolewa mwaka 2022.
“Hospitali yetu inaweza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje 58,319 na mwaka jana wagonjwa waliolazwa ni 6,787 akina Mama waliojifungua 1,421 tuna mpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya hospitali hapa,”amesema Dk.Luzila.

Pia, aepongeza Rais Samia kwa kuamua kutengeneza miundombinu ya barabara ya kufika katika hospitali hiyo kwa kiwango cha lami, ambayo Zabuni yake imetengazwa jana, na kuomba mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo uharakishwe, kwa kupatikana Mkandarasi na ujenzi uanze mara moja na kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.
Aidha,ameipongeza Bodi hiyo, na kuahidi kwamba watafanya kazi kwa kushirikiana kwa ukaribu, ili kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo Dk.John Majigwa, amesema watafanya kazi kwa nguvu zote ili kuinua huduma za afya Hospitalini hapo.

Bodi hiyo mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, kabla ya kuziduliwa wajumbe walipewa mafunzo mbalimbali ya usimamizi wa hospitali hiyo.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Katibu Tawala wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizundua Bodi Mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John akizungumza kwenye uzinduzi wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza kwenye uzinduzi wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.John Majigwa.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya Dk.Fadhili Kibaya akizungumza kwenye uzinduzi wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP.Salum Hamduni (kulia) akimkabidhi vitendea kazi Makamu Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Wajumbe wapya wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wakitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464