KATAMBI ASIMULIA KISA CHA MAMA MMOJA ALIYENUSURIKA KIFO KUSOMBWA NA MAJI YA MTO,KILIVYOMPA MACHUNGU YA KUTAFUTA FEDHA ZA DHARURA KUJENGA DARAJA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu,amesimulia kisa cha mama mmoja mkazi wa Uzogole Manispaa ya Shinyanga ambaye alinusurika kifo kwa kusombwa na maji ya mto kutokana na eneo hilo kukosa daraja kwa kipindi kirefu ambapo maji hayo yalikosa uelekeo na kuvamia shambani kwake.
Katambi ametoa simulizi hiyo leo Februari 28,2025 wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Kata ya Chamaguha,akiwaeleza namna alivyotekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa asilimia 100 ndani ya miaka yake Minne ya Ubunge.
Amesema kipindi anaingia kwenye Ubunge alikutana na tukio la Mama huyo kunusurika kifo wakati akilima shamba na mtoto wake,ambapo ghafla alishitukia maji yakianza kumzunguka huku mtoto akiwa amekimbia kuomba msaada,ndipo ikabidi apande juu ya mti ili awe salama kutosombwa na maji.
"Watu walipofika kutoa msaada walikuta maji ni mengi yakipita kwenye mto,ndipoikabidi wasubili na mama huyo alikaa juu ya mti masaa matatu mpaka yalipopungua ndipo wakamtoa,"amesema Katambi.
"Tukio hilo lilinihuzunisha sana na muda huo ndiyo nilikuwa nimeingia tu kwenye Ubunge,ikabidi nitafute fedha kwa kuongea na viongozi wa juu wa Tarura nitafanikiwa kupata pesa za dharura nikajenga daraja hilo la Uzogore kwenda Bugwandege ili maji yawe yanapita kwenye daraja na siyo kusambaa kwenye mashamba ya watu,na kuhatarisha maisha yao,"ameongeza Katambi.
Amesema baada ya kujenga daraja hilo,ikabidi afanye pia ziara ili kubaini madaraja ambayo ni hatarishi, na akatafuta pesa na yote ameyajenga likiwamo la hapo Chamaguha kwenda Kitangili.
Aidha,amesema katika sekta hiyo ya miundombinu ameitendea haki, na kwamba licha ya kujenga madaraja ambayo yalikuwa korofi, pia miundombinu ya barabara ameiimarisha, na barabara nyingi zinapitika tofauti na miaka ya nyuma kabla hajawa Mbunge.
Amesema baada ya mvua kunyesha baadhi ya miundombinu ya barabara kwa sasa imeharibika, na kwamba tayari wameshapata fedha sh.milioni 500 na zitafanyiwa matengenezo.
Amesema ndani ya miaka yake Minne ya Ubunge,amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo ya maji, umeme, barabara,elimu,pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege.
Mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Said Bwanga,amempongeza Mbunge Katambi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa asilimia 100.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anord Makombe,amewataka wana CCM kuendelea kuwa kitu kimoja ili wapate ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi Mkuu 2025 wa kuchagua Madiwani,Wabunge na Rais.
TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anord Makombe akizungumza.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akizungumza.
Mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Said Bwanga akizungumza.
Mkutano ukiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464