DC MTATIRO ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MKATABA UJENZI MRADI WA MAJI,ATAKA UIMARA WA MABOMBA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,ameshuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Lyagiti wilayani Shinyanga,kati ya Ruwasa na Mkandarasi.
Hafla hiyo ya utiaji saini mkataba huo wa ujenzi wa mradi wa maji,unaofahamika Buzinza,Mapingili,Mwamakala,Kimandaguli, na sasa upo awamu ya pili ambao utatekelezwa katika kijiji cha Lyagiti, imefanyika jana katika shule ya msingi Lyagiti na kushuhudiwa pia na wananchi wa kijiji hicho.
Mtatiro akizungumza kabla ya utiaji saini mkataba huo wa ujenzi wa mradi wa maji,amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake kubwa ya kumtua ndoo kichwani mwanamke, na kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya maji hapa nchini,huku akimsihi Mkandarasi ambaye anatekeleza mradi huo wa maji Lyagiti, kwamba aweke mabomba imara.
Amesema mradi huo unatumia fedha nyingi, hivyo anataka kuona unatekelezwa kwa kiwango bora na thamani ya fedha ionekane, pamoja na kuwekwa mabomba imara ili udumu kwa muda mrefu kuwa hudumia wananchi, na kuwaondolea adha ya ukosefu wa maji safi na salama kijijini humo na kumtua ndoo kichwani mwanamke.
“Ruwasa wakati wa utekelezwaji wa mradi huu wa maji, fanyeni ukaguzi wa mara kwa mara, na kuhakikisha vifaa ambavyo vinawekwa viwe imara na vyenye ubora zaidi, ili mradi uwe wa kudumu,”amesema Mtatiro.
Amewasihi pia wananchi, kwamba mradi huo utakapo kamilika kujengwa licha ya kwamba vitawekwa vituo vya kuchotea maji, bali na wenyewe wajitahidi kuvuta mabomba majumbani mwao, ili kutekeleza adhima ya Rais Samia ya kumtua ndoo kichwani mwanamke.
Aidha,ameonya kwamba wakati wa ujenzi wa mradi huo wa maji, kusije kuingizwa masuala ya siasa katikati, ili kutosababisha kusua sua, na kutolea mfano kuna Kata mmoja waliigiza siasa kwenye mradi kama huo na waliwachukulia hatua wote waliohusika, na kuonya katika mradi wa Lyagiti wasijaribu kufanya hivyo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela, amewasihi wananchi wa Kijiji cha Lyagiti, kwamba mradi huo waulinde na wasiuhujumu sababu ni mali yao, na pia washirikiane na Mkandarasi ikiwamo kulinda vifaa vya ujenzi.
Diwani wa Lyamidati Luhende Kawiza,ameshukuru kwa mradi huo wa maji, na kwamba wananchi wa Kijiji hicho walikuwa wanashida kubwa ya maji, na sasa tatizo lao linakwenda kutatuliwa.
Meneja Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA)wilaya ya Shinyanga Mhandisi Emael Nkopi, akisoma taarifa yake, amesema hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Shinyanga ni asilimia 78.8, na kwamba kati ya vijiji 126 vilivyopo wilayani humo,vijiji 75 vimepata huduma ya maji safi na salama, na bado miradi inaendelea kutekelezwa.
Amesema kwa upande wa ujenzi huo wa mradi wa majisafi na salama katika Kijiji cha Lyagiti, utekelezaji wake ni wa mwaka mmoja, wenye thamani ya sh.milioni 807, na utanufaisha wananchi wapatao 3,500.
Naye Mkandarasi ambaye anatekeleza ujenzi wa mradi huo wa maji Lyagiti Mhandisi Clemence Chagu Katobesi kutoka Kampuni ya Halem Construction Company Limited, ameahidi kwamba atautekeleza wa kiwango bora, pamoja na kuukamilisha ndani ya muda wa mkataba.
Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Lyagiti,wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo wa majisafi na salama kijijini humo, na kwamba wameshuhudia na wao ukisainiwa, na kuomba ukamilishwe kwa wakati, ili waanze kunufaika maji kutoka Ziwa Victoria.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Lyagiti baina ya Ruwasa na Mkandarasi.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Lyagiti baina ya Ruwasa na Mkandarasi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nicodemus Siamon,akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Lyagiti baina ya Ruwasa na Mkandarasi.
Diwani wa Lyabukande Luhende Kawiza,akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Lyagiti baina ya Ruwasa na Mkandarasi.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Shinyanga Mhandis Emael Nkopi akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Kijiji cha Lyagiti.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Lyagiti wilayani humo,baina ya Ruwasa na Mkandarasi.
Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Juliety Payovela (kulia)akikabidhia nyaraka na Mkandarasi Clemence Chagu Katobesi kutoka Kampuni ya Halem Construction LTD mara baada ya kumaliza kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Lyagiti wilayani Shinyanga.
Baadhi ya wanachi wa Kijiji cha Lyagiti wilayani Shinyanga wakishuhudia utiaji saini ujenzi wa mradi wa maji kijijini humo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464