MAKOMBE AHITIMISHA “HAPPYBIRTHDAY” YA MIAKA 48 YA CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anord Makombe,amehitimisha maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM katika wilaya hiyo.
Tarehe 29.1.2025 Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini kilizindua Maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama hicho Kata ya Mwawaza, na leo Februari 3,2025 kimehitimisha Maadhimisho hayo katika Kata ya Chamaguha, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama.
Makombe akizungumza wakati wa kuhitimisha Maadhimisho hayo, amewashukuru wananchi kwa kuendelea kukiamini chama hicho, na hata kukipatia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana 2024, huku akiwasihi pia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025, wakipigia kura nyingi ili kiendelee kushika dola na kuwaletea maendeleo.
“CCM kutimiza miaka 48 siyo haba, na kimefanya mambo makubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi,hivyo endeleeni kukiamini Chama, na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kapigeni kura nyingi kwa Rais Samia, Wabunge wa CCM pamoja na Madiwani, ili tuendelee kushika dola,”amesema Makombe.
Aidha, ametamka kwamba CCM wilaya ya Shinyanga Mjini wanaunga mkono Azimio la Mkutano Mkuu wa CCM taifa kwa kumpitisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na Mgombea mwenza Dk.Emmanuel Nchimbi, kuwa Mgombea pekee ambaye atagombea Urais kwa tiketi ya CCM kwenye uchaguzi Mkuu 2025 pamoja na Rais Dk.Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar.
Katika hatua nyingine, amewataka vijana kuchangamkia fursa ambayo imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ya kusoma bure katika Chuo cha HillForest hapa Shinyanga, kwa kusomea fani ya Hotel Menejment.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko, amekipongeza Chama cha Mapinduzi CCM chini ya Mwenyekiti wake Taifa Rais Samia, ambaye ametekeleza ilani ya CCM kwa asilimia 100 ndani ya utawala wake wa miaka 4, na kwamba katika Manispaa hiyo ametoa zaidi ya Sh.bilioni 11 na miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha, amesema katika Maadhimisho hayo, wamefanya mambo mbalimbali ya kijamii, ikiwamo kupanda miti,kutoa msaada kwa watoto yatima,kusalimia wagonjwa,kuzindua kituo cha bodaboda,kusajili wanachama,na kuwashukuru wananchi kuwapatia ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa
Chama cha Mapinduzi CCM kilianzishwa tarehe 5.2.1977 baada ya vyama viwili kuungana, Chama cha TANU na ASP ndipo ikazaliwa CCM na kwamba Februari 5,2025 kitakuwa kimefikisha miaka 48 tangu kuanzishwa kwake.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Anord Makombe akizungumza wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa CCM.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM.
Maadhimishi ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini yakiendelea.