VIJANA NA WASOMI MKOANI SHINYANGA, IGENI MFANO WA BBT KISHAPU - RC MACHA

VIJANA NA WASOMI MKOANI SHINYANGA, IGENI MFANO WA BBT KISHAPU - RC MACHA

Na. Paul Kasembo, NGOFILA - KISHAPU

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka vijana wasomi mkoani hapa kuiga mfano wa vijana wa Jenga Kesho yako Bora (BBT) waliopo Kata ya Ngofila wilayani Kishapu ambao waliamua kujitolea na kuitumia elimu na maarifa yao yote katika kusaidia wakulima na kuamua kulima mashamba yao ya mfano kwa wakulima ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa taaluma waliyoipata Chuoni na kwenye mafunzo maalum ya BBT.

Hayo ameyasema jana wakati wa ziara ya kukagua na kuhamasisha kilimo cha zao la pamba katika Kata ya Ngofila wilayani Kishapu ambapo ametembelea Kijiji cha Mwamanota, Idushi na Ngofila ambapo huko amekutana na vijana hao wenye ari, nguvu na moyo wa dhati wa kutumia elimu na muda wao wote katika mashamba ya wakulima na ya kwao ikiwa ni sehemu ya kujipatia kipato, kujiajiri na hivyo kuwa sehemu ya mfano na chachu kwa vijana wengine.

"Niwashauri vijana na wasomi wetu mkoani Shinyanga, njooni muige na kujifunza namna bora ya kujiajiri na kutumia vema nguvu, elimu na maarifa mliyonayo huku Kata ya Ngofila wilayani Kishapu ambapo kuna vijana wenzenu kutoka kundi la Jenga Kesho iliyo Bora ambao wameamua kujitolea na kutumia elimu, maarifa na muda wao kuwasaidia wakulima katika kilimo cha pamba na wao pia kulima mashamba ya mfano ikiwa sehemu ya kujiajiri na kuongeza pato binafsi," amesema RC Macha.

Aidha, RC Macha amesema kuwa kwa sasa atakuwa anapatikana zaidi vijijini ambako ndiyo walipo wakulima na kwamba atatumia muda mwingi zaidi kuhamasisha na kuwatia moyo wakulima wote ili kuhakikisha heshima na hadhi ya pamba mkoani Shinyanga inarejea kama ilivyokuwa hapo awali, kwani pamba (dhahabu nyeupe) ni sehemu ya utambulisho wa Mkoa wa Shinyanga.

Akitolea mfano wa shamba la Raphael Zengi mkulima wa Kijiji cha Ngofila ambaye msimu wa 2023/2024 alipata kilo 4605 kwa hekari 4 ambapo ni wastani wa kilo 1150 kwa hekari moja, RC Macha amesema huo ndiyo mlengo na nia ya Serikali ya kuhakikisha kila mkulima anapata kuanzia kilo 1000 au zaidi kwa hekari moja.

Na kwa mujibu wa Raphael anatarajia kuvuna kilo zaidi ya 1200 kwa kila hekari moja msimu huu wa 2024/2025 kwa kuwa ameboresha, amezingatia maelekezo ya wataalam na ameongeza eneo la kilimo chake, huku akiishukuru sana Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezssha kupata pembejeo zote muhimu tena kwa wakati jambo ambalo limewatia moyo na hamasa ya kulima zaidi pamba msimu huu.

Awali akitoa salamu za Wilaya kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi alisema kuwa kwa ujumla wakulima wanayo ari, nguvu na hamasa kubwa ya kulima na kwamba ujio wake utaongeza molari na kasi zaidi ya kulima ili mwisho wa siku lengo la kuongeza kipato kwao, kuimarisha uchumi na pato la Taifa liweze kufikiwa kwa pamoja.

RC Macha alimalizia ziara yake kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ambapo hapo pamoja na kuwaeleza dhamira ya ziara yake wilayani Kishapu lakini pia alipokea, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi hao huku akiwaahidi kuwa Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali sana na itaendelea kuwaletea maendeleo kupitia Sekta zake ambapo kila kijiji kimefikiwa kwa namna yake.

Kwa mujibu wa Mathias Nyanda ambaye ni Afisa Ugani Kilimo Kata alisema, Kata ya Ngofila yenye kaya 1619 ina Vijiji 5 ambavyo ni Ngofila, Kalitu, Inolelo, Mwamanota na Idushi pamoja na kilimo cha pamba, pia wananchi wake wanajishughulisha na kilimo cha mahindi, choroko, mtama, dengu, alizeti, mpunga na viazi vitamu huku pamba pekee ikiwa imelimwa takribani hekari elfu 25.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464