MASHINDANO YA KATAMBI U-17 CUP YAZINDULIWA RASMI

MASHINDANO YA KATAMBI U-17 CUP YAZINDULIWA RASMI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MWENYEKITI wa Jumuiya ya wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga John Siagi,amezindua rasmi mashindando ya Katambi U-17 CUP,huku akiwataka vijana kuonyesha vipaji vyao sababu michezo ni ajira.
Uzinduzi huo wa mashidano hayo umefanyika leo Februari 18,2025 katika Uwanja wa CCM Kambarage uliopo Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa michezo,ambayo yamefadhiliwa na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira,Vijana na watu wenye ulemavu na yatashirikisha Timu 16.

Siagi akizungumza wakati wa kuzindua mashindano hayo, amempongeza Mbunge Katambi kwa kuendelea kuunga mkono suala la michezo, ambalo lipo kwenye utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM, na amekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana katika Manispaa ya Shinyanga na hata baadhi yao kupata ajira.
“Vijana tumieni fursa ya mashindano hayo kuonyesha vipaji vyenu sababu kwa sasa michezo ni ajira, na shabiki namba moja wa michezo hapa nchini ni Dk.Samia Suluhu Hassan tangu ameingia madaraka amekuwa na dhamira ya kuinua Sekta ya michezo,”amesema Siagi.

“Natoa wito kwa vilabu vikubwa vya michezo hapa nchini waje mkoani Shinyanga kwenye mashindano haya ili waone vipaji vya vijana n ahata kupata wachezaji wa baadae katika timu zao,”ameongeza.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Samweli Jackson, amesema Mbunge Katambi anadhamira ya kuibua vipaji vya vijana, ndiyo maana amekuwa akianzisha mashindamo mbalimbali ya michezo pamoja na kufadhili, sababu anajua michezo ni ajira.

“Mashindano yaliyopita ya Dr.Samia/ Katambi Cup,yametoa ajira kwa kijana James Nhungo Machibula, ambaye amesajiliwa na Timu ya Simba “B” Under 20, akitokea Timu ya Mwamalili FC,” hivyo nawaomba vijana katika mashindano haya ya Katambi U-17 onyesheni vipaji vyenu,”amesema Samweli.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu wilaya ya Shinyanga Mjini (SHIDIFA)Joseph Assey, amempongeza Mbunge Katambi kwa kuthamini michezo na amekuwa mdau mkubwa, na kuomba aendelee kuwa na moyo huo huo ili kuibua vipaji vya vijana.

TAZAMA PICHA 👇👇
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga John Siagi akizungumza kwenye uzinduzi wa mashindano ya Katambi U-17 CUP.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shianyanga Mjini Samweli Jackson akizungumza kwenye uzinduzi wa mashindano ya Katambi U-17 CUP.
Mwenyekiti wa SHIDIFA Wilaya ya Shinyanga Mjini Joseph Assey akizungumza kwenye uzinduzi wa Mashindano ya Katambi U-17 CUP.
Walimu wakikabidhiwa Jezi na Mipira kwa ajili ya vijana Under 17 kuanza mashindano hayo.





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464