Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi akizungumza wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Ndala, Masekelo na Mwawaza 

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi akizungumza wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Ndala, Masekelo na Mwawaza
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko akizungumza wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Ndala, Masekelo na Mwawaza
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imewataka wanachama wake kutoridhika na idadi ya wanachama waliopo, bali waendelee kuhamasisha kujiunga kwa wanachama wapya na kuwasajili kwa mfumo wa kielektroniki.
Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi, wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Masekelo, Ndala na Mwawaza, leo Ijumaa, Februari 21, 2025.
"Tusiridhike na wanachama tulionao, naomba tuendelee kuongeza wanachama wapya. Na wanachama hawa wasajiliwe kwenye mfumo wa kielektroniki na tulipie ada ya kadi zetu," amesisitiza Kibabi.
Aidha, Bi. Kibabi amekumbusha umuhimu wa kufanya vikao vya kikatiba na kikanuni ndani ya jumuiya, akiongeza kwamba vikao vya kujenga chama ni muhimu zaidi kuliko vile vinavyoshughulikia migogoro ya watu binafsi.

Doris Kibabi
“Tukumbuke kuwa uhai wa chama ni kufanya vikao. Fanyeni vikao vya kikatiba na kikanuni kwenye jumuiya zenu kwa sababu vikao vinajenga. Hali kadhalika viongozi mliochaguliwa naomba muongoze kama inavyotakiwa, msifanye vikao vya kushughulikia watu,fanyeni vikao vya kujenga chama”,amesema Kibabi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, amesema CCM itaendelea kuwa chama imara, akiongeza kuwa ni chama kisichoendeshwa kwa vitisho, kinyume na vyama vingine vya siasa.
"CCM siyo chama cha vitisho vitisho kama wale wenzetu. Wale wenzetu wana siasa za vitisho vitisho, njooni CCM tukijenge chama chetu," amesema Mrindoko.
Pia, ametoa wito kwa jamii kutowachekea watu wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto, akisisitiza umuhimu wa kulinda watoto na kuwapa elimu bora kwa manufaa ya kesho yao.
“Tusiwachekee hawa wahuni wanaobaka na kulawiti watoto, tuwalinde watoto wetu, tuwaache watoto wasome, tusiruhusu wachezewe hawa watoto. Tunataka watoto wasome, kesho na kesho kutwa watatusaidia”,amesema Mrindoko.
“Msiruhusu watoto walale na wageni, siku hizi kuna vibabu vya hovyo vinawageuza watoto wake zao na kuwafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia”,ameongeza.
Wajumbe hao wa Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini wakiwa kwenye ziara yao ya kata kwa kata katika Jimbo la Shinyanga Mjini, wametembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa Kivuko kinachounganisha kata ya Masekelo na Ibinzamata na kuagiza Mkandarasi anayetekeleza mradi huo uliotekelezwa kwa shilingi Milioni 100 kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa kivuko hicho.
Pia wametembelea na kukagua ujenzi unaoendelea wa maboma mawili ya shule ya msingi Msufini B iliyopo katika mtaa wa Mlepa kata ya Ndala.
Ziara hiyo ya kata kwa kata inaonyesha juhudi kubwa zinazofanywa na Jumuiya ya Wazazi CCM katika kuimarisha chama na kuendeleza maendeleo ya kijamii katika Wilaya ya Shinyanga Mjini.