KATAMBI AAHIDI BARABARA YA HOSPITALI YA KOLANDOTO KUJENGWA KIWANGO CHA LAMI


KATAMBI AAHIDI BARABARA YA HOSPITALI YA KOLANDOTO KUJENGWA KIWANGO CHA LAMI

Na Marco Maduhu SHINYANGA

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu,ameahidi kuipambania Barabara ya Hospitali ya Kolandoto kujengwa kiwango cha Lami.
Katambi amebainisha hayo leo Februari 25,2025 wakati akizungumza na wananchi wa Kolandoto kwenye mkutano wa hadhara wa kuelezea yale ambayo ameyatekeleza ndani ya miaka yake Minne ya Ubunge pamoja na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

Amesema kero ambayo wananchi wameitoa ya ubovu wa barabara ya hospitali ya Kolandoto, kwamba barabara hiyo atahakikisha inawekewa lami,sababu mwaka wa fedha uliopita waliiombea fedha lakini hawakupata.
"Ni aibu barabara Hospitali ya Kolandoto yenye Ubia na Serikali kuwa mbovu, na Hospitali hii ina historia kubwa sana,na nimeipima ni kilomita 1.2 hivyo nitahakikisha inawekewa lami,"amesema Katambi.

Aidha,amesema katika Kata hiyo ya Kolandoto mambo mengi ameyatekeleza ikiwamo kusambaza mtandao wa maji ikiwamo kijiji cha Mwanumbi,Mwang'obeko na Gharamba maeneo ambayo hayakuwa na maji kabisa lakini sasa yapo.
Amesema pia wamepata fedha sh.bilioni 195 kwa ajili ya kusambaza mtandao wa maji kwa wananchi wote wa Manispaa ya Shinyanga.

Amesema pia,kwa upande wa Zahanati ya Mwamagunguli tayari zimeshapatikana fedha sh.milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba,huku akibainisha kwamba changamoto nyingi ambazo zilikuwa zikiikabili Kata ya Kolandoto nyingi amezitatua.
Nao baadhi ya wananchi wa Kolandoto akiwamo Bruno Mlemi,waliwasilisha kero yao ya ubovu wa barabara ya Hospitali ya Kolandoto na kumuomba Mbunge Katambi alitatue tatizi hilo.

Waliwasilisha kero zingine zikiwamo za ukosefu wa maji na umeme kwenye baadhi ya vitongoji, na kuomba nazo zitatuliwe, ambapo kwenye Mkutano huo Wataalamu kutoka kwenye sekta husika walizijibu kuwa miradi hiyo ipo kwenye hatua za utatuzi.
Mbunge Katambi,anaendelea na ziara yake ya Kata kwa Kata kwa kufanya mikutano ya ndani pamoja na hadhara kwa kuzungumza na wananchi kuwaeleza yale ambayo ametekeleza ndani ya miaka yake Minne ya Ubunge.

TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu,akizungumza na wananchi wa Kolandoto.
Diwani wa Kolandoto Mussa Andrew akizungumza kwenye Mkutano huo.
Wananchi wa Kolandoto wakiwa kwenye Mkutano wa Mbunge Katambi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464