WAZIRI WA UCHUKUZI PROF.MAKAME MBARAWA ATEMBELEA UJENZI UWANJA WA NDEGE SHINYANGA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI MAAGIZO YA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA


WAZIRI WA UCHUKUZI PROF.MAKAME MBARAWA ATEMBELEA UJENZI UWANJA WA NDEGE SHINYANGA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI MAAGIZO YA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

WAZIRI wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa,ametembelea kukagua ujenzi wa upanuzi uwanja wa ndege shinyanga, kusimamia maagizo ambayo yalitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,kuwa uwanja huo hadi kufikia Aprili ufungwe Taa, na ndege zianze kutua nyakati za usiku.
Mbarawa amefanya ziara hiyo Jana Februari 20,2025 kwa kuzungumza na wasimamizi wa ujenzi wa Uwanja huo wa Ndege,Wakandarasi,pamoja na kutembelea kuona ujenzi wa miundombinu ya uwanja huo.

Amesema ujenzi wa uwanja huo wa ndege baadhi ya miundombinu ambayo ni ya muhimu tayari imekamilika, ikiwamo barabara ya kutua na kuruka ndege (Runway),na kuwaagiza wasimamizi wa ujenzi wa uwanja huo na TANROADS,kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi aagize malighafi na kuzifunga Taa kwenye uwanja huo ili kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Majaliwa.
“Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Februari 16 alipofika kwenye ujenzi wa uwanja wa Ndege Shinyanga, aliagiza ifikapo April Mosi, uwanja huu uwekewe Taa ili uanze kutumika nyakati za usiku, hivyo TANROADS hakikisheni Mkandarasi anaweka “Order ya Material”ili Taa hizo zifungwe na kutekelezwa kwa agizo la Waziri Mkuu,”amesema Prof.Mbarawa.

Aidha, amempongeza pia Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha jitihada zake za kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo wa ndege unafanikiwa pamoja na viwanja vingine vitatu kikiwamo cha Sumbawaga,Tabora na Kigoma,na kwamba haikuwa kazi rahisi, lakini sasa hivi viwanja hivyo vina kwenda kukamilika na kutoa huduma ya usafiri wa Anga kwa wananchi.
Amewapongeza pia Wakandarasi kwa uvumilivu wao, kwamba ujenzi wa upanuzi wa uwanja huo wa Ndege Shinyanga ulisainiwa mwaka 2017, lakini katikati ukasuasua, ndipo Rais Samia akasimama kidete ili ujengwe, na ujenzi wake Rasmi ukaanza mwaka 2023, na mpaka sasa wameendelea nao na wapo hatua za mwisho kuukamilisha.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)Lugano Mwinuka, amesema uwanja huo wa Ndege wa Shinyanga, zitakuwa zikitua ndege za masafa ya karibu zenye uwezo wa kubeba abiria 70-76 pamoja na kutumika kama dharura na utakuwa”feeder airport”.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amemshukuru Rais Samia juu ya ujenzi wa uwanja huo wa Ndege, kwamba amefungua fursa za kiuchumi mkoani humo.

Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Donatus Binamungu, amesema ujenzi wa upanuzi wa uwanja huo wa ndege Shinyanga umefikia asilimia 74, na kwamba barabara ya kutua ndege imekamilika kwa asilimia 100 na ndege zinaweza kutua mchana, na kueleza watamsimamia Mkandarasi kuagiza Taa ili zifungwe na kuanza kutumika nyakati za usiku hadi ifikapo mwezi Aprili.

TAZAMA PICHA👇👇
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa akizungumza katika Uwanja wa Ndege Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza katika Uwanja wa Ndege Shinyanga.
Mwakilishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)Lugano Mwinuka, awali akiwasilisha taarifa kwa Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Donatus Binamungu, awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa uwanja huo wa Ndege Shinyanga.
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa akikagua ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Shinyanga.
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa akiangalia mchoro wa ujenzi wa upanuzi Uwanja wa Ndege Shinyanga.
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa akiendelea kukagua ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege Shinyanga.
Awali Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa (kulia)akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha alipowasili kwenye ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Shinyanga.
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa (kulia)akisalimiana na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samweli Mwambungu, alipowasili kwenye ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Shinyanga.
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa akisalimiana na Wakandarasi wa ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Shinyanga.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464