
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Bodi mpya ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imefanya ziara ya kutembelea utekelezaji mradi wa mtambo wa kuchakata tope taka unaolenga kuboresha huduma za usafi wa mazingira kwa wananchi wa Shinyanga huku ikipongeza hatua zilizofikiwa katika upanuzi wa mtambo huo wa kisasa ambapo kwa sasa umefikia asilimia 98 ya utekelezaji.
Ziara hiyo imefanyika leo Februari 13, 2025 na bodi ya (SHUWASA) kufanya ukaguzi wa mradi huo uliopo kata ya Kizumbi ndani ya manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo ,Mwenyekiti wa bodi hiyo Bi Mwamvua Jilumbi ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) kwa kufanya upanuzi wa eneo la mradi huo na kuepuka kusimama kwa shughuli za uchakataji wa tope taka kulingana na ufinyu wa eneo uliokuwepo hapo awali huku akimpongeza mkandarasi kwa hatua nzuri ya utekelezaji wa upanuzi wa mradi huo ulipofikia.
“Kama bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA tumeridhishwa na utekelezaji huu wa mradi unaofanya na SHUWASA kwa kweli thamani ya fedha inayotumika tunaiona na tuipongeze menejimenti ya SHUWASA kwa kuamua kuongeza eneo hili la mradi wa uchakataji wa tope taka ni matumaini yetu sasa mradi huu utaendelea kufanya kazi vizuri, lakini pindi mradi huu utakapo kamilika nitoe rai ukusanyaji wa mapato kwa uangalifu mkubwa kwa sababu mapato yakipatikana itawezesha mamlaka kufanya miradi mingine ya kimaendeleo na manufaa makubwa”, amesema Bi Mwamvua.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi huo Msimamizi wa uborehaji wa mradi kutoka (SHUWASA) Mhandisi Wilfred Julias amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 98 na kubainisha kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza uwezo wa mtambo ili kukidhi mahitaji.
“Mtambo ulkuwa na uwezo wa kuchakata mita za ujazo 40 za tope taka kwa siku lakini baada ya upanuzi kukamilika utafikia hadi mita za ujazo 100 kwa siku”, amesema Mhandisi Wilfred.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Shinyanga SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola amesema upanuzi wa mtambo huo utakwenda kukuza pato la ukusanyaji lakini pia kukidhi mahitaji ya ukusanyaji wa tope taka kutoka majumbani lengo likiwa ni kuendelea kuweka manispaa ya Shinyanga katika hali ya usafi na kuendeleza heshima ya kuwa manispaa inayoongoza kwa usafi nchini.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464