Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika kuwaletea maendeleo wananchi, huku ikiwasihi wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla kutokubali kuathiriwa na maneno ya baadhi ya watu wanaobeza jitihada za Rais Samia.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Jumanne Februari 18, 2025, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, alipokuwa katika ziara yake na wajumbe wa kamati ya utekelezaji wilaya ya Shinyanga Mjini, ziara iliyofanyika katika kata za Mwamalili na Old Shinyanga.
Ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa kimkakati wa kutembelea kata zote za Jimbo la Shinyanga Mjini, ambapo lengo kuu ni kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM, kufanya tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuangalia hali ya uhai wa chama, na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo hayo.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mrindoko amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na kutambua juhudi zake za kuboresha ustawi wa taifa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko
"Msikubali kupotoshwa, nchi hii imejengeka. Hawa wanaokuja kubeza leo wametoka wapi? Tumshike mkono Mama Samia, tumpe mitano tena, amefanya mambo mazito, tusimame pamoja naye. Mama huyu amefanya mambo mazuri sana. Naomba msimame imara, hakuna mtu wa kuwayumbisha na kuwatoa kwenye mstari mkamuacha Samia,” amesema Mrindoko.
Amesema pia ni muhimu kupuuza watu wanaobeza mafanikio ya Rais Samia, akitaja baadhi yao kama "washamba" wanaopuuza maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika sekta muhimu kama vile miundombinu, elimu,maji, umeme na afya.
"Tuwapuuze hawa washamba wanaopuuza kazi nzuri zinazofanywa na Mama Samia katika sekta mbalimbali. Watanzania tuendelee kuwa macho na kushirikiana kwa pamoja ili kutimiza malengo ya maendeleo," amesema Mrindoko.
Pia, amezungumzia umuhimu wa kulinda watoto dhidi ya vitendo vya ubakaji na ulawiti, akisema: "Hawa wanaolawitiana na kusagana ni dhambi kubwa kwa Mungu. Tukatae hii tabia ya watoto wetu kuchezewa chezewa, tukabiliane na hawa wanaochezea watoto wetu, wanaolawiti na kubaka watoto wetu."
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Dorice Kibabi, amesisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa wanachama wa CCM, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kibabi pia amehamasisha wananchi kujiunga na chama na kulipa ada ya uanachama CCM, akisema kuwa uhai wa chama unatokana na michango ya wanachama ikiwemo kulipia kadi ya uanachama.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa tangu aingie madarakani ambapo alikuta miradi mingi mikubwa ya kimkakati ambayo sasa tayari imekamilika, mingine ikiwa katika hatua za mwisho za kukamilika.
Mhandisi Jumbe ameongeza kuwa, Rais Samia amekuwa akifanya juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara, sekta ya afya, elimu, na kutoa mikopo kwa makundi maalum kama watu wenye ulemavu, vijana na wanawake.Mhandisi James Jumbe
“Rais Samia ni mtu anayetaka maendeleo, amekuwa akiboresha miundombinu, uboreshaji huu wa miundombinu ya barabara unasaidia kwa kiwango kikubwa sana kuhakikisha uchumi wetu unakua kwa kasi kubwa. Rais Samia pia amewezesha katika sekta ya afya, vifaa tiba, majengo ya hospitali, vituo vya afya, zahanati. Kwenye elimu ameboresha mikopo ya chuo kikuu, elimu ya sekondari, walimu wanaajiriwa,” amesema Jumbe.
“Mheshimiwa Rais Samia ni mtu ambaye ana maono, tumeona mchakato kuhusu Dira ya taifa, hiyo yote ni kuhakikisha Mhe. Rais Samia anatengeneza taifa ambalo lina dira thabiti itakayosaidia kizazi kilichopo na kijacho”,ameeleza Mhandisi. Jumbe
Mhandisi Jumbe amefafanua kuwa, Rais Samia anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa, ndiyo maana wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walimpendekeza kwa kauli moja kama mgombea wa Urais kupitia CCM katika uchaguzi Mkuu 2025.
“Mheshimiwa Rais Samia anatekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa na amefanya kazi pasipo kuchoka ndiyo maana mkutano mkuu wa CCM wajumbe walipitisha azimio la mkutano mkuu kumpitisha kuwa ndiye Mgombea pekee wa Urais kupitia CCM.
Hakupitishwa kwa sababu yeye ni mwanamke au kwa sababu tu yeye ni mkuu wa nchi ana vyombo vya ulinzi na usalama lakini utekelezaji wa Ilani, watu waliridhika nao na ndiyo maana wajumbe wa mkutano mkuu, kupitia maoni ya wanachama mbalimbali walipendekeza Dkt. Samia Suluhu Hassan awe mgombea Urais lakini pia Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza ambaye amefanya kazi kubwa katika chama hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Mhe. Nchimbi ni mchapakazi, muungwana, mwenye heshima, mstahimilivu. Kwa hiyo ukiangalia huo muungano (combination) ya Dkt. Samia na Dkt. Nchimbi hakuna mashaka kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tunaenda kushinda kwa kishindo,” ameongeza Mhandisi Jumbe.
“Kwa hiyo, kama tulivyoshirikiana kwa umoja katika uchaguzi wa serikali za mitaa, na mimi naendelea kuwaomba ndugu zangu, wanachama, wanajumuiya ya wazazi, na jumuiya nyingine za chama, tuungane kwa nguvu moja katika chaguzi zijazo. Uzuri ni kwamba, tutakuwa na wagombea tunaowafahamu, na hivyo tutaangalia ni kiongozi gani anayefaa kutuongoza. Ipo wazi kabisa kwamba mitano ni kwa Mheshimiwa Rais Samia na mgombea mwenza, Dkt. Emmanuel Nchimbi, huku nafasi zingine zikigombewa kwa utaratibu ulioainishwa na chama ili kupata wagombea wanaozingatia maslahi ya umma. Lengo letu ni kuhakikisha chama kinaendelea kushika dola, tushirikiane kwa nguvu, tuendelee kujenga chama, tuunge mkono Rais wetu na viongozi wa chama, na tupate ushindi mkubwa,” amesema Jumbe.
Mhandisi Jumbe amesema uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa wa ushindi mkubwa kwa CCM, akisisitiza umoja wa wanachama katika kuhakikisha ushindi mkubwa.
Jumbe amewahamasisha wanachama wa CCM na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana na kupigania maendeleo, akisema: “Tunatakiwa kuwa makini kwenye malezi ili kutengeneza taifa bora. Tujitahidi kuwa karibu na watoto wetu, tuzungumze nao, kwa sababu wanapitia changamoto mbalimbali ili kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji ambavyo vinaanzia ngazi ya familia.”
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, akizungumza katika ziara yake na wajumbe wa kamati ya utekelezaji wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Mwamalili na Old Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, akizungumza katika ziara yake na wajumbe wa kamati ya utekelezaji wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Mwamalili na Old Shinyanga.


