Akizungumza na wananchi na waandishi wa habari ,Mhe. Mboni amesisitiza kuwa maeneo haya yanajivunia rutuba ya ardhi, hali nzuri ya mazingira, na unafuu wa uzalishaji wa mazao hayo, hivyo ni fursa ambayo haiwezi kupuuziliwa mbali.
"Hii ni nafasi nzuri ya kuwekeza, kupata mavuno bora, na kujenga uchumi wa wilaya nzima, Nawakaribisha Ushetu kwa ajili ya Kilimo cha Tumbaku na Pamba na Msalala kwa ajili ya Kilimo cha Mpunga", amesema.
Mhe. Mboni amefafanua kuwa kilimo cha tumbaku na pamba kimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa wilaya ya Kahama, huku kilimo cha mpunga kikitarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya chakula na biashara katika halmashauri ya Msalala.
Ametoa wito kwa wakulima na wawekezaji kuungana na serikali ili kufanikisha miradi hii ya kiuchumi, ambayo pia inaongeza ajira kwa vijana na kuongeza kipato cha familia.
Mhe. Mboni ameongeza kuwa wilaya ya Kahama iko tayari kutoa ushirikiano wa karibu kwa wakulima, kuanzisha mashamba ya kisasa, na kuboresha mifumo ya usambazaji wa mbegu bora, mbolea, na teknolojia ya kisasa ya kilimo.
"Kilimo ni nguzo muhimu ya uchumi wa wilaya yetu, na tunataka kuona Kahama inajivunia kuwa kioo cha kilimo cha kisasa, na hivyo kuboresha maisha ya watu wetu," amesema Mhe. Mboni kwa furaha.
Kwa hiyo, ni wakati wa kuchangamkia fursa hii ya kipekee na kujiunga na juhudi za maendeleo za Wilaya ya Kahama, huku mwelekeo wa kilimo cha kisasa ukionekana kuwa mkombozi kwa wakulima na wanajamii wote.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464