Na MWANDISHI WETU,
DODOMA.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo Rasmi (National Informal Sector Scheme-NISS) iliyoboreshwa inalenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi waliojiajiri wenyewe kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mhe. Ridhiwani alisema hayo mwanzoni mwa wiki hii wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ustawi na Maendeleo ya Jamii, iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma.
Amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa skimu hiyo imetengenezwa vizuri na ina faida kubwa kwa jamii kwani inatoa kinga dhidi ya majanga kama uzee, ulemavu, ugonjwa hivyo amewataka wabunge kuwa mabalozi wazuri wa skimu hiyo.
“Waheshimiwa wabunge nyinyi ni wawakilishi wa wananchi mna wajibu wa kuwaeleza Watanzania kuhusu skimu hii pamoja na faida zake ili waweze kujiunga na kuchangia kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye,” amesema Mhe. Ridhiwani.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema skimu hiyo imeanzishwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi waliojiajiri wenyewe katika shughuli za kiuchumi na kuwa wanufaika ni pamoja na wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji wadogo wa madini, mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine wote.
Bw. Mshomba amesema mwanachama anapaswa kuchangia kiasi kisichopungua shilingi 30,000 ambapo atanufaika na fao la matibabu yeye mwenyewe au shilingi 52,200 ambapo atanufaika na matibabu yeye na familia yake. Amesema mwanachama anaweza kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki au mwezi na kuwa anapaswa kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) kuwasilisha michango.
Akizungumzia namna ya kuchangia katika skimu hiyo, Meneja Mifumo wa NSSF, Bw. Mihayo Mathayo amesema wamerahisisha uchangiaji kupitia akaunti ya benki au wakala kwa kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo (control number), kupitia simu ya kiganjani (Mitandao yote) kwa kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo (control number).
Awali, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Fatma Toufiq ameipongeza NSSF kwa kuboresha skimu hiyo ambayo inaenda kuwa mkombozi wa wananchi waliojiajiri wenyewe kwa kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko