RCC SHINYANGA YARIDHIA MAPENDEKEZO 8 YA MATUMIZI BORA YA ARDHI,
Na. Paul Kasembo,
KAMATI ya Ushauri ya Mkoa wa Shinyanga (RCC) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Anamringi Macha ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kauli moja imeridhia mapendekezo 8 juu ya matumizi bora ya ardhi yenye lengo la kuwezesha ufikaji katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji ndani na nje ya mkoa.
Mapendekezo yaliyoridhiwa na RCC ni pamoja na kuboresha miundombinu ya mtandao wa barabara ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma, kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji itakayosaidia ongezeko la mazao ya kilimo na viwanda vya usindikaji, kuboresha na kuwezesha miundombinu ya taaluma ambayo itasaidia upatikanaji wa Taasisi za Elimu ya juu pia kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo ya Miji na Vijiji.
Mapendekezo mengine ni urejeshaji wa ardhi iliyoharibika na uhifadhi wa mazingira ambao utapunguza athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, kujenga na kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya afya itakayoimarisha upatikanaji wa hduma za afya kirahisi, kujenga viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya kilimo na mifugo itakayokuza uchumi na kuongezeka kwa kipato, sambamba na kujenga miundombinu ya kuchakata madini ambayo itaongeza kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla
Akiwasilisha mapendekezo hayo Jonas Masanja kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ndg.Joseph Mafuru alisema kuwa kupitisha taarifa hii kwenye RCC ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria kabla ya kumfikishia Waziri mwenye dhamana na iweze kuingia kwenye bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kuridhiwa kwa mapendekezo hayo kunakwenda sanjari na kuufanya Mkoa wa Shinyanga kuwa Kituo cha Usindikaji wa Mazao ya Kilimo na Kitovu cha Madini Tanzania vitu ambavyo vinatajwa kuwa chechemuzi katika uchumi wa wananchi, kuboresha maisha yao na kuongeza pato la Taifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464