Na Mwandishi Wetu - Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameipongeza timu inayosimamia mchakato wa ajira za Ualimu kwa namna wanavyoendesha zoezi hilo kwa uadilifu na ufanisi.
Mhe. Simbachawene amesema hayo leo tarehe 22 Februari, 2025 wakati alipotembelea na kukagua timu inayosimamia mchakato wa ajira za Ualimu Chuo Kikuu Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani Morogoro.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaita ofisini kwake Dodoma kwa mazungumzo Viongozi wa vijana waliojitambulisha kwenye andiko lao kuwa ni “Non Employed Teachers Organisation (NETO)” wenye umoja wao kupitia mitandao ya Kijamii.
“Nimesoma Makala yao yenye kichwa cha habari Ombi la Wahitimu wa Ualimu Vyuo mbalimbali Nchini kati ya mwaka 2015-2023 kwa Serikali, andiko lao ni zuri na linaeleweka ingawa linahitaji ufafanuzi zaidi, hivyo ninatoa wito kwa vijana hao kuja ofisini Dodoma kwa mazungumzo” alisisitiza Mhe. Simbachawene.
Aliongeza kuwa amewasiliana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda na Viongozi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na wamekubalina kushiriki mazungumzo hayo wakati kundi hilo litakapokuwa tayari.
Mhe. Simbachawene amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya Falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya), hivyo kwa moyo wa upendo amewakaribisha ili kupata maridhiano katika jambo wanaloona haliko sawa.
Aidha, amesema kuwa kuanzia tarehe 14 Januari hadi terehe 24 Februari, 2025 Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (UTUMISHI), Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Afya; Tume ya Utumishi wa Walimu, Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma inaendesha usaili wa kada za Ualimu.
“Usaili huu una lengo la kujaza nafasi elfu kumi na nne mia sita na arobaini na nane (14,648) zilizotolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini” alifafanua Mhe. Simbachawene.
Naye, Msimamizi wa Kituo hicho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bibi. Hilda Kabissa amesema kuwa zoezi linaendelea vizuri na Sekretarieti ya Ajira inaendesha usaili wa aina tatu, Usaili wa kuandika (Aptitude Test), Usaili wa vitendo (Practical) na Usaili wa mahojiano ya ana kwa ana (Oral Interview) kwa kuzingatia mahitaji ya kada au nafasi inayotakiwa kujazwa.





