Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe Wiswa, amechangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Kituo cha Afya Kambarage Manispaa ya Shinyanga.
Mchango huu unalenga kuimarisha usalama wa wagonjwa na watoto wachanga waliozaliwa katika kituo hicho.
Mhandisi Jumbe amekabidhi mifuko hiyo ya saruji leo, Jumamosi, Februari 22, 2025, wakati wa ziara ya Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambapo wamekagua maendeleo katika Kituo cha Afya Kambarage na ujenzi wa barabara ya Kenyatta-Karena kwenye kata hiyo.
Ziara hiyo pia imejumuisha mazungumzo na wanachama na viongozi wa CCM kutoka Kata ya Kambarage, Lubaga na Mjini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mifuko ya saruji, Mhandisi Jumbe amesema, "Nimeamua kutimiza ahadi yangu kutoa mifuko hii ya saruji ili kuimarisha ulinzi katika Kituo cha Afya Kambarage. Kamati ya Kituo hiki iliniletea ombi la kuchangia ujenzi wa uzio na mimi nimelijibu kwa vitendo. Kituo hiki kipo kwa ajili ya wagonjwa mbalimbali na wengi ni akina mama na watoto, na tunahitaji kuwalinda kwa kila hali."
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi James Jumbe Wiswa (kushoto), na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko wakikabidhi mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika kituo cha afya Kambarage
“Niipongeze kamati ya Kituo cha afya Kambarage kwa namna ambavyo wanajitahidi kutoa michango mbalimbali, Mwenyekiti wa Kamati aliniandikia barua tangu mwaka jana akaniambia wana ujenzi wa uzio wa kituo hiki, na mimi nikamuahidi nitamchangia kama alivyoeleza, zoezi letu tumekuwa tukiliahirisha mara kwa mara lakini mara ya mwisho nikamwambia kuwa kwa kuwa mimi ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji Wazazi na ukizingatia kituo hiki cha afya kwa kiwango kikubwa kipo kwa ajili ya wazazi hasa akina mama ni muhimu tuungane ili kuhakikisha kunakuwa na usalama,” amesema Mhandisi Jumbe.
Mhandisi James Jumbe Wiswa
"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejitahidi sana kuboresha sekta ya afya, ametoa vifaa tiba, amejenga majengo ya kisasa, amenunua vifaa vingi vya kisasa vya gharama kubwa, ambapo tulikuwa tunatumia gharama kubwa sana kuvipata kwenye sekta binafsi. Mama Samia ni mama mwenye watoto, anajua kadhia ambazo akina mama wanapitia. Sisi kama wadau wa maendeleo, na mimi pia ni mfanyabiashara, tunapaswa kujitolea kwa ajili ya jamii yetu,” ameongeza Mhandisi Jumbe.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha jitihada kubwa kuboresha sekta ya afya nchini, na yeye kama mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi, ameamua kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia katika ujenzi wa uzio akisema "Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amejitahidi kuboresha sekta ya afya, ametoa vifaa vya kisasa na kujenga majengo bora.
“Kwa hiyo, nimeona ni vyema kumuunga mkono Rais Samia kwa juhudi zake kubwa. Kama wadau, ametufanyia mazingira rafiki ya kufanya shughuli zetu na tumeweza kulipa kodi bila kusumbuliwa. Hivyo, tunapaswa kutoa kile tunachopata kusaidia jamii yetu. Na nawaasa wafanyabiashara wa Shinyanga, tunao wengi, wajitolee kusaidia. Nafurahi wapo ambao wametoa mchango wao, uzio huu ni kidogo kama wote tungeshirikiana, ukishiriki kuchangia uzio huu maana yake unashiriki kulinda uhai wa mwanadamu ambao mwenyezi Mungu ametupatia. Hatupaswi kuweka mazingira hatarishi kwa akina mama wanaokuja kupata huduma, lazima tuwajibike na kuwalinda,” amesema Mhandisi Jumbe.
Na sisi wana Shinyanga tunamuunga mkono kwa vitendo, na vitendo vyenyewe ni kushiriki shughuli za maendeleo na kutatua changamoto ambazo zinakumba jamii yetu. Mchango huu pia ni ishara ya kuunga mkono azimio la Mkutano Mkuu CCM kumteua Rais Samia kugombea tena Urais akiwa na mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi. Hii ni ishara ya kumpongeza kwa juhudi zake” ,ameeleza Mhandisi Jumbe.
Viongozi wa Kituo cha Afya Kambarage, Mwenyekiti wa Bodi Adolf Nzwanzungwanko na Mganga Mfawidhi Dkt. Ernest Magula, walimshukuru Mhandisi Jumbe kwa mchango wake na kusema kuwa uzio huo utasaidia kuimarisha usalama hasa wakati wa usiku, hivyo kurahisisha huduma za afya kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, akiwa katika kata za Kambarage, Mjini na Lubaga Mhandisi Jumbe pamoja na wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini wamewahamasisha wanachama wa CCM kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
"Kazi yetu kama makada wa CCM ni kuyasemea mambo mazuri yaliyofanywa na Rais Samia. Tunataka Rais Samia apate ushindi mkubwa katika uchaguzi Mkuu mwaka huu, ni mama mwenye huruma na ameimarisha amani, umoja, na mshikamano",amesema Jumbe.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, amesisitiza kuwa chama kinapaswa kuungwa mkono kwa sababu kimeendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa Shinyanga.

