VIONGOZI WA DINI KEMEENI MAOVU –ASKOFU NGUSA

 

Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu ya Wabaptisti Tanzania Mchungaji Barnabas Ngusa

Mgeni Rasmi ,Muhandisi wa mradi wa umeme jua uliopo katika kata ya ngunga wilayani Kishapu  George Jimisha 

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA   

VIONGOZI wa dini wametakiwa kutumia nyumba za ibaada kutenda haki na kukemea vitendo viovu,ili kuwawezesha waumini wao kwenda kutenda haki kwenye jamii pamoja na kuliombea taifa linapoelekea kufanya uchaguzi mkuu mwaka huu ili amani iendelee kutawala.

Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa jumuiya kuu ya wabaptisti Tanzania mchungaji Barnabas Ngusa wakati akiweka jiwe la msingi katika  kanisa la Baptisti lililopo ngwamishoni kata ya bubiki wilayani kishapu mkoa wa Shinyanga,lililiojengwa kwa nguvu za washirika na wafadhili  ambapo amesema watu wanapokosa hofu ya Mungu wanafanya matukio ya kikatili.

“Niwaombe na kuwasihi ndugu zangu tutumie nyumba za ibada vizuri kuwafundisha watu neno la Mungu  mnapokusanyika katika nyumba za ibada msianze kusengenyana na kusemana vibaya badala yake wachungaji muwasaidie waumini ili wawe watenda haki na wenyewe”amesema Ngusa

Katika hatua  nyingine Askofu Ngusa ameiomba serikali kuharakisha utatuzi wa mgogoro unaoendelea katika kanisa hilo unaohusisha viongozi waliomaliza muda wao  na wa sasa hali iliyopelekea baadhi ya  makanisa katika mkoa wa Mbeya na Kigoma kufungwa huku akiomba serikali kuyafungua makanisa hayo wakati mchakato wa suluhu ukiwa unaendelea ili waumini  waendelee kuabudu katika mazingira rafiki.

“Nitumie fursa hii kumuomba waziri wa mambo ya ndani Inocent Bashingwa kama lilivyo jina lake kuwa ni mtu asiyekuwa na hatia kwenye hili atende haki kwani kuna kamati zimeundwa na polisi na uchunguzi unaendelea”lakini kuna wenzetu  bado wanaendelea kuchukua baadhi ya maeneo ambayo ni mali ya kanisa hilo pasipo kusubiri uchunguzi huo ukamilike” amesema Ngusa   

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo muhandisi wa mradi wa umeme jua uliopo katika kata ya ngunga wilayani Kishapu  George Jimisha ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kanisa hilo , amewaomba waumini  kuendelea kuliombea taifa  pamoja na uchaguzi mkuu wa rais,wabunge na madiwani utakaofanyika mwaka huu ili wapatikane viongozi wenye hofu ya Mungu.

Nao baadhi ya waumini na viongozi wa kanisa hilo wakaeleza hatua ya ujenzi ilipofikia huku wakihitaji nguvu zaidi  kutoka kwa wadau mbalimbali ili kukamilisha kabisa ujenzi wa kanisa hilo ili waumini wa maeno hayo waweze kumuabudu mwenyezi Mungu katika mazingira rafiki.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464