WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO, HAMISHIENI NGUVU KWENYE UONGEZAJI THAMANI WA MAZAO - RC MACHA.
Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka wafanyabiashara ndogondogo kubadilika na kuelekeza nguvu, maarifa na mitaji katika biashara mpya ya uongezaji thamani kupitia mazao (kilimo) kwani sehemu kubwa ya biashara ndogondogo zinaonekana kutokwenda kwa kasi ambayo wengi wao wanaitarajia huku akisisitiza kuwa njia rahisi, salama, ya uhakika na kweli ni kilimo.
RC Macha ameyasema hayo leo tarehe 14 Februari, 2025 wakati akizindua na kukabidhi Vitambulisho vya Kidigitali kwa Wafanyabiashara ndogondogo 172, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Machinga na wanachama wao ambao ndiyo walengwa wa hafla hiyo.
"Niwatake sasa wafanyabiashara ndogondogo hapa Shinyanga muanze sasa kubadilisha mwelekeo kutoka katika biashara za mazoea za hapa mjini kati, na badala yake mhamishie nguvu, maarifa na mitaji yenu katika biashara ya uongezaji thamani mazao ambapo huko mkajikite kwenye kilimo hata cha bustani kwa kuanzia," amesema RC Macha.
Akitoa mfano wa mafanikio kupitia Kikundi cha Jipage kilichopo Kata ya Kishapu, wilayani Kishapu ambao wao waliamua kuelekeza nguvu katika kuongeza thamani ya mazao kwa kulima bustani ambapo kwa mwaka 2023 walilima na kupata tikiti elfu 11 ambazo waliuza Tzs. Milioni 22 na baada ya kutoa gharama za uendeshaji walipata faida ya Milioni 11 na mwaka 2024 walilima na kupata tikiti elfu 25 zilizotoa Tzs. Mil. 75 na walipotoa gharama za uendeshaji wakabakiwa na Mil 48 kama faida.
Uzinduzi wa vitambulisho vya kidigitali kwa wafanyabiashara wadogowadogo mkoani Shinyanga ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa kwa Wizara husika lengo ni kuwatambua na kuifanya mifumo iweze kusomana na hivyo kupelekea urahisi wa kuwezesha itakapohitajika huku wito ukitolewa kuendelea kuhamasisha na kujitokeza kujoandisha ili lengo la kuwainua kiuchumi kwa pamoja liweze kufikiwa na Serikali.
Akitoa salamu za wanachama wake, Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Shinyanga ndg. Mupinda Bwesa amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali na kuwathamini machinga ambapo pamoja na bitambulisho vya kidigitali ambavyo vinakwenda kuwasaifia sana kupata fursa, lakini pia aliwezesha kujengwa kwa Ofisi zao Mikoa yote ukiwemo na Shonyanga na sasa wanamuombea zaidi ili awndelee kuwahudumia watanzania wote wakiwemo wao machinga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464