
Mbunge Stanislaus Mabula
Na Tonny Alphonce,Mwanza
Jumla ya shilingi Bilioni 1.3 imetolewa Kwa vikundi 87 vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu wa wilaya ya Nyamagana kijini Mwanza.
Akizungumza na vikundi hivyo mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amevipongeza vikundi hivyo 87 vilivyofanikiwa kupata mkopo katika awamu hii ya kwanza na kuwataka kutumia mikopo hiyo Ili kubadili hali za Maisha yao na ya watu wanaowazunguka.
"Mikopo hii ikawe na tija kwenu kwa kuendeleza biashara mlizonazo lakini pia kubadili mfumo wa maisha yenu kama ulikuwa unakula mlo mmoja Sasa ule milo mitatu"alisema Makilagi.
Aidha mkuu wa wilaya Makilagi amevitaka vikundi hivyo vilivyopewa mkopo vihakikishe vinafanya marejesho wa mujibu wa mikataba waliyosaini.
"Dawa ya deni ni kulipa maana fedha hii mliyopewa sio ya kwenu peke yenu Kuna wenzenu hawajapata hivyo hakikisheni mnarudisha Ili na wenzenu waweze kukopa"alisema Makilagi
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanislaus Mabula ameipongeza serikali Kwa kurejesha mikopo hiyo iliyokuwa ikisubiriwa Kwa hamu kubwa na wananchi.
"Nachoweza kusema mikopo hii ikawe chachu kwenu katika kuhakikisha kwamba inafungua fursa na ukurasa mwingine lakini ikawe sehemu ya kujitegemea na kujishughulisha kiuchumi"alisema Mabula
Mabula amewataka wale ambao hawajapata mikopo hii katika awamu hii ya kwanza kuendelea kujipanga na kuhakikisha wanatimiza vigezo na masharti Ili nao waweze kupata mikopo ya awamu ijayo ambapo fedha zaidi ya Bilioni 2 zitatolewa.
Mikopo ya asilimia 10 ambayo hutolewa kutoka katika mfuko wa mapato ya ndani yahalmashauri ilianza kutolewa nchini mwaka 1995 kabla ya kusimamishwa mwaka 2023 Ili kutafuta mwongozo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464