KATAMBI ATOA NOTI MASHINDANO U-17 CUP,SHIDIFA WAANZA KUONA VIPAJI
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, ametoa pesa shilingi milioni 1 kwa ajili ya kuendeleza mashindano ya “Katambi U-17 Cup” ambayo yanaendelea katika viwanja mbalimbali.
Mashindano haya yalizinduliwa rasmi Februari 18, 2025, katika Uwanja wa CCM Kambarage na Mwenyekiti wa Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, John Siagi, ambayo yanashirikisha timu 16.
Katibu wa Mbunge, Samweli Jackson, amekabidhi kiasi hicho cha pesa leo, Februari 9, 2025, kwa Kamati ya Utendaji ya Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA) kwa niaba ya Mbunge Katambi.
Amesema kuwa Mbunge Katambi alishatoa awali Shilingi milioni 4, na sasa ameongeza milioni 1 ili kuendeleza mashindano haya, akiwa na dhamira ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana.
Ameongeza kuwa, kwa sasa mpira wa miguu ni ajira, akitaja mfano wa kijana James Nhungo ambaye alisajiliwa na Timu ya Simba “B” Under 20 kupitia mashindano ya Dr. Samia/Katambi Cup.
Samweli amekishukuru Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA) kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha mashindano hayo yanaenda vizuri,huku akiwasihi pia marefa wachezeshe kwa haki bila upendeleo wa timu yoyote.
"Mbunge Katambi anapenda sana michezo na amekuwa akianzisha mashindano mbalimbali ili kuibua vipaji vya vijana. natoa wito kwa wadau wa michezo kuhudhuria mashindano haya ya U-17 ili kuona vipaji vya vijana," amesema Samweli.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA)Joseph Assey, amempongeza Mbunge Katambi kwa kuthamini michezo,amesema kwa mashindano ambayo yanaendelea hivi sasa ya Katambi U-17 Cup, tayari wameshaanza kuona vipaji vya vijana.
Katibu wa Mbunge Katambi, Samweli Jackson wapili (kutoka kulia)akikabidhi sh.milioni 1 kwa SHIDIFA kwa ajili ya kuendeleza mashindano ya Katambi U-17 CUP.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464