MADIWANI SHYDC WAPITISHA PENDEKEZO KUGAWA JIMBO LA SOLWA,KUWA NA MAJIMBO MAWILI YA UCHAGUZI
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, wamepokea,kujadili na kupitisha pendekezo la kugawa Jimbo la Solwa,kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Solwa na Itwangi.
Wamepitisha mapendekezo hayo leo Machi 11,2025 kwenye Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani, kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa ya pendekezo la kugawa Jimbo la Solwa. kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi, Solwa na Itwangi, kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
Awali Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Oscar Lupavila, akiwasilisha taarifa kwa Madiwani kwa niaba ya Mkurugenzi, amesema Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuligawa Jimbo la Solwa na kutoa vigezo vyake 10, ambapo pia madiwani wanapaswa kujadili na kupitisha mapendekezo ya kuligawa jimbo hilo.
Amesema Jimbo la Solwa kwa sasa linakadiriwa kuwa na Watu 503,167 kufikia 2025,ambapo kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Jimbo hilo lilikuwa na Watu 468,611.
Amesema Jimbo la Solwa likigawanywa, ambapo Solwa iitakuwa na Watu 309,821 na Itwangi 193,346, na kwamba Kati ya vijiji 126 na vitongoji 856, kuwa Solwa itakuwa na vijiji 68 na vitongoji 478,huku Itwangi itakuwa na vijiji 58 na vitongoji 378.
“Jimbo la Solwa kwa sasa lina ukubwa wa Kilomita za Mraba 4,212, likigawanywa, Solwa itabaki kuwa na Kilomita za Mraba 2,573.29, na Jimbo la Itwangi litakuwa na Kilomita za Mraba 1,638.71,”amesema Oscar.
Ameendelea kueleza kuwa,Jimbo la Solwa litakuwa na Tarafa ya Nindo pamoja na Kata 12, ambapo Itwangi itakuwa na Tarafa mbili ya Itwangi na Samuye, na kwamba Samuye ina Kata 4,Itwangi Kata 10 ambapo jumla zitakuwa Kata 14.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nicodemus Simon,amesema mapendekezo hayo ya kuligawa Jimbo la Solwa ni mchakato wa awali, na kwamba mara baada ya madiwani kumaliza kuyapitisha,yatawasilishwa tena kwenye Kikao cha Kamati cha Ushauri wilaya (DCC), na kisha kwenda kwenye Kikao cha Kamati cha Ushauri Mkoa (RCC), na baada ya hapo Katibu Tawala Mkoa atawasilisha kwa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi.
“Vigezo vyote ambavyo vimetolewa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi kuligawa Jimbo hili la Solwa tumekidhi,tuombe Mungu ligawanywe, na nitafurahi kuona Madiwani mkijitokeza kugombea Ubunge katika Jimbo hili jipya la Itwangi sababu nyie ndiyo mnajua zaidi changamoto za wananchi,”amesema Simon.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela,ameipongeza Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi, kwa nia ya kuligawa Jimbo hilo la Solwa, na kwamba itasaidia kusogeza huduma kwa wananchi.
TAZAMA PICHA👇👇
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nicodemus Simon akizungumza kwenye kikao cha baraza.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Sterwart Makali akizungumza kwenye baraza la madiwani.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela akizungumza kwenye baraza la madiwani.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwenye baraza la madiwani.
Uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Oscar Lupavila akiwasilisha taarifa kwenye baraza la madiwani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464