STAND UNITED YAVUNA POINT 3 KWA MTIBWA SUGAR,YARAMBA MAMILIONI YA JUMBE

STAND UNITED YAVUNA POINT 3 KWA MTIBWA SUGAR,YARAMBA MAMILIONI YA JUMBE

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

TIMU ya Stand United ya Mkoani Shinyanga (Maarufu Chama la Wana) imeibuka na ushindi kwa goli moja kwa bila, dhidi ya Timu ya Mtibwa Sugar katika Ligi ya Championship na kuondoka na Point 3.
Mchezo huo umechezwa leo Machi 17,2025 katika Uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga, na kuhudhuriwa na mashambiki pamoja na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro.

Mchezo huo ambao ni wa kufuzu kushiriki Ligi kuu ya Tanzania Bara, ambapo kipindi cha kwanza ulianza na kasi kubwa na Stand United kufanikiwa kupata penati dakika ya 8, mkwaju uliopigwa na Mchezaji Omari Ramadhani,goli ambalo lilidumu hadi dakika ya 90.
Kocha wa Timu ya Stand United Chama la wana Masoud Juma, amesema vijana wake walifuata maelekezo yake na ndiyo maana wameibuka na ushindi huo, na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kushiriki kucheza Ligi kuu ya Tanzania Bara.

“Ushindi huu umetupa Morali hivyo tutaendelea kupambana katika michezo yetu iliyosalia kwa kuhakikisha tunapata ushindi na tunawaomba wadau wa michezo pamoja na mashabiki waendelee kutu “Support”,”amesema Juma.
Kocha wa Timu ya Mtibwa Sugar Awadhi Juma, amesema mipango yao katika mchezo huo wamefeli na wenzao wametumia makosa wakapata penati na waibuka na ushindi na kwamba wanajipanga katika mchezo ujayo.

Naye mdau wa michezo Jackline Isaro, akimwakilisha Mhandisi James Jumbe,amesema waliahidi kutoa fedha sh.milioni 2 endapo Timu hiyo ikaibuka na ushindi, na kwamba amekabidhi fedha hizo kwa Capteni wa Timu hiyo Babilas Chitembe, pamoja na sh. 200,000 kwa goli ambalo wameshinda.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Samweli Jackson, amesema Mbunge huyo naye amechangia kiasi cha sh.milioni moja, ili kuiunga mkono Timu ya Stand United katika ushindi wake wake huo.

Kufuatia Mchezo huo Timu ya Stand United inafikisha point 49 na kusalia nafasi ya 3, ambapo inakuwa na pointi sawa na Mbeya City ambayo inashika nafasi ya pili kwa tofauti ya magoli,huku Mtibwa Sugar ikisalia katika nafasi yake ya kwanza kwa point 54.

TAZAMA PICHA👇
Mdau wa michezo Jackline Isaro akikabidhi fedha sh.2,200,000 kwa Timu ya Stand United mara baada ya kuichapa bao moja Timu ya Mtibwa Sugar, kwaniaba ya Mhandisi James Jumbe.
Katibu wa Mbunge Katambi, Samweli Jackson akikabidhi sh.Milioni Moja kwa Timu ya Stand United mara baada ya kuichapa bao moja Timu ya Mtibwa Sugar.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akiongoza hamasa katika mchezo wa Timu ya Stand United na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa CCM Kambarage.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464