RC MACHA AMPONGEZA RAIS SAMIA KUTIMIZA MIAKA MINNE YA UTAWALA WAKE


RC MACHA AMPONGEZA RAIS SAMIA KUTIMIZA MIAKA MINNE YA UTAWALA WAKE

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amempongezaRais Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza miaka minne ya utawala wake, na kwamba katika mkoa huo ametoa kiasi cha fedha sh.Trilioni 1 na kutekelezwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
RC Macha.

Macha amebainisha hayo leo Machi 19,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari,siku ambayo Rais Samia aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania awamu ya sita, mara baada Hayati Rais John Pombe Magufuli kufariki dunia Machi 17,2021.

Amesema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua nafasi ya Hayati Magufuli,ameitendea haki kwa kuchapa kazi ya kuwatumikia wananchi, na kwamba katika mkoa wa shinyanga ndani ya miaka yake minne, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa.
“Leo Machi 19 ni siku ambayo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania awamu ya sita, mara baada ya Hayati Rais John Pombe Magufuli kufariki dunia Machi 17,2021, Mkoa wa Shinyanga tunampongeza Rais Samia kutimiza miaka minne ya utawala wake, na amefanya kazi kubwa kuwatumikia Watanzania,”amesema Macha.

“Tukizungumzia tu kwa mkoa wa Shinyanga ndani ya miaka minne ya Rais Samia, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa ukiwamo ujenzi wa uwanja wa ndege ambao miaka mingi ulishindwa kukamilika wenye thamani ya sh.bilioni 52,”ameongeza Macha.

Amesema kwa upande wa miundombinu ya barabara, barabara nyingi zimejengwa, na sasa barabara ya kutoka Kahama kwenda Kakola ya kilomita 73 inajengwa kwa kiwango cha lami sh.bilioni 101.

Amegusia pia miradi ya maji, kwamba wananchi wengi wamefikiwa na huduma hiyo, na bado miradi mingine inaendelea kutekelezwa, na hadi ifikapo mwishoni wa mwaka 2025 wananchi wa vijijini watakuwa na maji kwa asilimia 85.

Amesema kwa upande wa umeme katika vijiji 506 vya mkoa huo tayari vyote vina umeme, na kwamba sasa hivi unapelekwa ngazi ya vitongoji, huku akimpongeza pia Rais Samia kwa kupigania matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ameongeza kuwa,kwa upande wa huduma za afya,halmashauri zote za mkoa huo zina hospitali za wilaya,pamoja na kuikamilisha hospitali ya rufaa ya mkoa huo, na sasa wananchi wanapata huduma za kibingwa hapo hapo Shinyanga.

Amesema kwa upande wa elimu, shule nyingi mpya zimejengwa za sekondari na msingi, pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa kwa shule ambazo zilikuwa na idadi nyingi ya wanafunzi, pamoja na kuendelea kutoa fedha za elimu bila malipo.

“Mungu aendelee kumpigania afya njema Rais Samia, ili aendelee kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo,”amesema Macha.

Amesema pia wanamuombea Hayati Rais John Pombe Magufuli ampumzike kwa Amani, na kwamba katika mkoa huo wa Shinyanga wataendelea kuyaenzi mambo mema ambayo aliyafanya katika taifa hili.

Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga,kwa nyakati tofauti wamemombea Hayati Rais Magufuli apumzike kwa Amani, huku wakimpongeza Rais Samia kwa kuvaa viatu vyake na kusimamia utekelezwaji wa miradi ya maendeleo, ikiwamo ya kimkakati kama vile Reli ya SGR, na daraja la Magufuli.

Hayati Rais John Pombe Magufuli,alikuwa Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2021, alipofariki dunia Machi 17 mwaka huo katika Hospital ya Mzena Jijini Dar es salaam kwa maradhi ya moyo, na kisha aliyekuwa Makamu wake wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuchukua kiti hicho, na kuapishwa Machi 19 na sasa amefikisha miaka minne ya utawala wake.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464