SHIRIKA LA LIFE WATER INTERNATIONAL TANZANIA LAWAONDOLEA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI SAFI NA SALAMA WANANCHI WA KIJIJI CHA BUGOGO
SHIRIKA la Lifewater International Tanzania,limetekeleza mradi wa maji safi na usafi wa mazingira katika Kijiji cha Bugogo Kata ya Mwamala wilayani Shinyanga, na kuwaondolea wananchi wa kijiji hicho adha ya ukosefu wa maji safi na salama.
Mkurugenzi wa shirika hilo Devocatus Kamara, akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi huo wa maji jana Machi 18,2025 pamoja na kukabidhiwa rasmi kwa wananchi, amesema utanufaisha wananchi 2,584.
Amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Agost 2022 na kukamilika Novemba 15,2024 kwa gharama ya Shilingi milioni 425.1, kwa kushirikiana pia na Ruwasa ambao wamechangia sh.milioni 2.7, pamoja na wananchi kuchangia nguvu kazi ikiwamo kuchimba na kufukua mitaro sawa na thamani y ash.milioni 37.5.
“Lengo la mradi huu ni kuwawezesha wakazi wa kijiji cha Bugogo,shule na zahanati kupata huduma ya majisafi na salama ndani ya umbali usiozidi mita 400 sawa na wastani wa kutumia dakika 30 kwenda kituo kwenye kituo cha kuchotea maji na kurudi nyumbani, ambapo tumejenga vituo 14,”amesema Kamara.
Amesema mradi huo chanzo chake cha maji ni kisima kirefu chenye kina cha mita 115 m na kinauwezo wa kutoa maji lita 12,000 kwa saa, na wamejenga tangi lenye ujazo wa lita elfu 60, na mtandao huo wa maji urefu wake ni kilomita 19,479.
Amesema mradi huo utakabidhiwa kwa wananchi wenyewe kupitia Chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO) ambao watauendesha pamoja na kuunganisha wateja wa majumbani.
Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum, amewapongeza wadau hao wa maendeleo kwa kushirikiana na serikali kutatua tatizo la ukosefu wa majisafi na salama kwa wananchi wa jimbo hilo, na kwamba utakapokamilika mradi wa Tindepackage kuwa kati ya vijiji 126 vya wilaya ya shinyanga vijiji 109 vikakuwa na maji na kusalia 17 tu.
Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi wa mradi huo wa majisafi na salama Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amewapongeza wadau hao Shirika la LifeWater International,kwa kuendelea kutatua changamoto ya ukosefu wa majisafi na salama,huku akiwasihi wananchi wautunze mradi huo pamoja na kuulinda.
“Mradi huu wa maji ni mkubwa sana, nampongeza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajenda yake hii ya kumtua ndoo kichwani mwanamke, na sasa tunaona miradi mingi ya maji inatekelezwa,pongezi pia kwa Mbunge Ahmed kwa kutafuta wadau hawa na anafaya kazi kubwa ya kuwatumia wananchi,”amesema Mtatiro.
Nao wananchi wa Kijiji cha Bugogo akiwamo Flora Masanja, wamesema mradi huo wa maji,umewasaidia sana kuondokana kuamka nyakati za usiku kufuata maji vijiji jirani pamoja na kutopoteza muda wa kufanya shughuli za kiuchumi.
Aidha,katika hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum alikabidhi Hati ya makabidhiano ya mradi huo wa maji kwa chombo cha wato huduma ya maji ngazi ya jamii CBWSO.
Uzinduzi huo wa mradi wa maji katika Kijiji cha Bugogo ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya maji 2025, yenye kauli mbiu isemayo”Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa uhakika wa maji”
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Bugogo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji Kijiji cha Bugogo.
Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji Kijiji cha Bugogo.
Diwani wa Mwamala Hamisi Masanja akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji Kijiji cha Bugogo.

Mkurugenzi wa Shirika la Life Water International Tanzania mkoani Shinyanga Devocatus Kamara akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa maji Kijiji cha Bugogo.

Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum akikabidhi Hati ya Mradi wa Maji Kijiji cha Bugogo kwa CBWSO, ambao ndiyo watausimamia mradi huo.

Mwanamke Bahati Zengo akielezea namna walivyokuwa wakipata shida kutokana na ukosefu wa maji kwenye Kijiji hicho cha Bugogo na sasa shida hiyo hawana tena.
Awali Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akikata utepe kuzindua mradi wa maji Kijiji cha Bugogo wilayani humo.
Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum akikata utepe kufungua jiwe la msingi.
Ufunguzi wa jiwe la msingi ukiendelea kwa ajili ya kuzindua mradi wa maji Kijiji cha Bugogo.
Uzinduzi wa mradi wa maji Kijiji cha Bugogo ukiendelea.
Muonekano wa mradi wa maji Kijiji cha Bugogo.
Tangi la Maji.
Picha za pamoja zikipigwa.