KAMATI YA BUNGE PIC YATEMBELEA MRADI WA MAJI MALAMPAKA-MALYA UNAOSIMAMIWA NA KASHWASA

KAMATI YA BUNGE PIC YATEMBELEA MRADI WA MAJI MALAMPAKA-MALYA UNAOSIMAMIWA NA KASHWASA

Na Marco Maduhu,SIMIYU

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC)imetembelea mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji ya Ziwa Victoria,kwenda katika Miji ya Malampaka na Malya,utakaonufaisha wananchi 131,057.
Ziara hiyo imefanyika leo Machi 20,2025 kwa kutembelea mradi huo ili kuona hatua za utekelezaji wake,ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama- Shinyanga KASHWASA,kwa kushirikiana na MAUWASA na RUWASA Kwimba, unaotekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya M/s Shanxi Constrution Engineering Corporation and Mineral Company.

Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Patrick Nzamba, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi Mhandisi Joshua Mgeyekwa,amesema upanuzi wa mradi huo wa maji unaanzia Hungumalwa wilayani Nkwimba, eneo ambalo lipo bomba kuu la usafirishaji wa maji ya Ziwa Victoria.
Amesema kuanzia Hungumalwa litalazwa bomba la kusafirisha maji katika Miji ya Malampaka na Malya, na kwamba katika Miji hiyo itajengwa mifumo ya usambazaji maji pamoja na maunganisho mapya takribani 4,000.

Amesema ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 24, na umeanza kutekelezwa kuanzia Februari 21,2024 na utakamilika Februari 20,2026 kwa gharama ya sh.bilioni 20.8 na unagharamiwa na serikali kwa asilimia 100.
“Mradi huu utakapokamilika unakadiriwa kunufaisha wakazi wapatao 131,057 wa Miji ya Malampaka na Malya pamoja na Vijiji 16, na kuongeza hali ya upatikaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 61 hadi 90,”amesema Mhandisi Nzamba.

Aidha,amesema hali ya utekelezwaji wa mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 18, na kwamba Mkandarasi ameshalipwa sh.bilioni 3.1 na anadai sh.bilioni 1.5 madai ya hati ya kwanza na yapili na hati hizo za madai zimekwisha wasilishwa Wizara ya Maji kwa hatua za malipo.
Amesema mradi huo kwa sasa unakabiliwa na changamoto ya kuchelewa kwa fedha za utekelezaji, na kuathiri malipo kwa Mkandarasi na kusababisha utekelezwaji wake kusuasua, na kuwa nyuma kwa asilimia 36 ikilinganishwa na muda ambao umefikia kwa sasa.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Augustino Vuma,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekelezwa mradi wa maji, ambao utawaondolea adha ya ukosefu wa maji wananchi wa Malampaka na Malya.
Amesema kwa tatizo la uchelewa kwa fedha za malipo ya Mkandarasi,kwamba wao kama Kamati hiyo ya Bunge watakwenda kukaa pamoja na Wizara ya Maji na fedha kulijadili,huku akiwasihi pia KASHWASA kufuatilia fedha hizo ili mradi huo ukamilike kwa wakati, ili wananchi wapate huduma ya maji.

“Fedha hizi zitakapokuja KASHWASA msimamieni Mkandarasi autekeleze mradi huu kwa viwango bora, na udumu muda mrefu kuwa hudumia wananchi,”amesema Augustino.

Nao baadhi ya wananchi wa Malampaka akiwamo Anna Maltini, amesema wanahamu ya kupata maji hayo ya kutoka Ziwa Victoria, na kuomba mradi huo ukamilishwe kwa wakati ili waondokane na tatizo la kufuata maji umbali mrefu.

TAZAMA PICHA 👇👇
Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA Mhandisi Patrick Nzamba akisoma taarifa ya mradi wa maji.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Augustino Vuma, akizungumza mradi huo wa maji.
Mwananchi Anna Maltini akizungumza mradi huo.
Baadhi ya wananchi wa Malampaka.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464