RUWASA KISHAPU WAHITIMISHA MAADHIMISHO WIKI YA MAJI,WANANCHI WASISITIZWA KUTUNZA MIUNDOMBINU NA VYANZO VYA MAJI

RUWASA KISHAPU WAHITIMISHA MAADHIMISHO WIKI YA MAJI,WANANCHI WASISITIZWA KUTUNZA MIUNDOMBINU NA VYANZO VYA MAJI

Na Marco Maduhu,KISHAPU

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)wilayani Kishapu,wamehitimisha maadhimisho ya wiki ya maji wilayani humo,huku Mkuu wa wilaya hiyo Peter Masindi akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Nyenze-Ng’wanh’olo utakaonufaisha wananchi 2,345 na kusisitiza utuzwaji wa miundombinu na vyanzo vya maji.
Maadhimisho hayo kiwilaya yamefanyika leo Machi 22,2025 katika Kijiji cha Ng’wanh’olo wilayani Kishapu.

Masindi akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya wiki ya maji,kwanza amewapongeza RUWASA wilayani humo kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi,na kwamba Kishapu ya sasa siyo ile ya zamani sababu maeneo mengi wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

Amesema maji ndiyo kila kitu kwa maisha ya binadamu,hivyo ni vyema wakayaheshimu pamoja na kutunza miundombinu yake na vyanzo vya maji.

“Maisha yetu kila siku yanahitaji maji, hivyo ni vyema wananchi mtunze vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ikikiwamo kilimo kando vya vyanzo hivyo, na msitake miti hovyo pamoja na uchomaji wa moto ili tutunze uoto wa asili,”amesema Masindi.
Amewasihi pia wananchi kwamba maji hayo wayatumie kwa faida ikiwamo kufanya kilimo cha umwagiliaji, pamoja na kupanda miti kwa wingi, ili kurudisha uoto wa asili na hata kupata mvua za kutosha.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Francis Manyanda ambaye ni Diwani wa Mwadui Luhumbo, amesema awali wananchi wa wilaya hiyo walikuwa na shida kubwa ya maji, lakini sasa hivi maeneo mengi yanapata maji.
“Mkuu wetu wa wilaya ya Kishapu leo ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Nyenze-Ng’wanh’olo, vijiji ambavyo vilikuwa na adha kubwa ya maji, lakini sasa hivi wanapata maji, tunawapongeza sana RUWASA,”amesema Manyanda.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu Shija Telezu,akizungumzia Mradi huo wa Maji,Nyenze-Ng’wanh’olo amewasihi wananchi kwamba wautunze,ili upate kuwa hudumia kwa kipindi kirefu.
Kaimu Meneja wa RUWASA wilayani Kishapu Mhandisi John Lugembe, amesema hali ya upatikanaji kwa sasa wilayani humo ni asilimia 65.2,na kwamba bado miradi mingine ya maji inaendelea kutekelezwa.

Amesema kwa upande wa mradi wa maji Nyenze-Ng’wanh’olo ambao umewekewa jiwe la msingi na Mkuu wa wilaya, kuwa ulianza kutekelezwa Februari 2024 kwa gharama ya sh.milioni 445.04, na kwamba kuwa licha ya kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi ujenzi wake umefikia asilimia 98.
Amesema mradi huo chanzo chake ni Maji ya Ziwa Victoria, na mtandao wake wa bomba ni kilomita 2.67,una vituo vitatu vya kuchotea maji na unanufaisha wananchi wapatao 2,345, na utekelezaji wake upo kwa awamu ya kwanza.

Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ng’wanh’olo akiwamo Milembe Joseph, wamesema mradi huo wa maji ni mkombozi kwao, kutokana na adha kubwa ambayo walikuwa wakiipata kwa kuamka majira ya usiku kufuata maji umbali mrefu na hata kupoteza muda wa kufanya shughuli za kiuchumi.

Kaulimbi ya maadhimisho ya maji 2025 inasema ”Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa uhakika wa Maji”

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi akizungumza kwenye kufunga maadhimisho ya wiki ya maji wilayani Kishapu.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu akizungumza.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Francis Manyanda akizungumza.
Kaimu Meneja RUWASA wilaya ya Kishapu Mhandisi John Lugembe akisoma taarifa.
Afisa Maendeleo wa RUWASA Neema Mwaifuge akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi akikata Utepe kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji,Nyenze-Ng'wanh'olo.

Moja ya kituo cha kuchotea maji katika mradi wa maji Nyenze-Ng'wanh'olo.
Maadhimisho ya kufunga wiki ya maji yakiendelea wilayani Kishapu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464