BUTONDO:SERIKALI INAWATHAMINI SANA VIONGOZI WA DINI

BUTONDO:SERIKALI INAWATHAMINI SANA VIONGOZI WA DINI

Na Marco Maduhu,KISHAPU

MBUNGE wa Kishapu Boniphace Butondo, amesema serikali ina wathamini na kuwategemea sana viongozi wa dini katika udumishaji wa Amani na kusababisha kufanyika kwa shughuli za maendeleo.

Amebainisha hayo jana wakati akikabidhi kiasi cha pesa shilingi laki tatu kwa Katibu wa Bakwata wilaya ya Kishapu kwa ajili ya kufanikisha ununuaji wa gari la ofisi ya Bakwata.

Mbunge Butondo (kushoto),akikabidhi fedha Bakwata.

Amesema serikali bila ya viongozi wa dini haiwezi kufanya shughuli za maendeleo kwa wananchi, sababu bila kuwapo na Amani hapa nchini hakuna kitu ambacho kinaweza kufanyika, na ndiyo maana inawathamini na kuwategemea na hata Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anawapenda sana viongozi hao.

“Serikali inathamini sana mchango wa viongozi wa dini hapa nchini, hasa kwa kuhakikisha Amani inaendelea kutwala,na bila Amani huwezi kufanya hata shughuli za maendeleo,”amesema Butondo.
“Hivi karibuni mlikuwa na Maulid lakini mimi sikuwepo na mkawa na mchango wa kuchangisha upatikanaji wa gari la Bakwata,na alikuwapo Katibu wangu akaniambia tu ameahidi kuchangia sh.laki tatu, na leo nina wakabidhi fedha hizo ili muongezee mpate gari ambalo litasaidia kuwafikia vizuri waumini na kuwapatia neno la Mungu,”ameongeza.

Naye Katibu wa Bakwata wilaya ya Kishapu Athuman Ally, amemshukuru Mbunge huyo kwa kutoa mchango huo wa fedha, kwamba licha ya kutokuwepo siku ya tukio, lakini amekuwa muungwana na kutoa kiasi hicho cha fedha ambacho kitawasaidia kuongeza kwenye ununuaji wa gari lao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464