KATAMBI ATOA MKWANJA MNONO KWA TIMU YA STAND UNITED IKIICHAPA MTIBWA SUGAR NA KUVUNA ALAMA 3 KAMBARAGE

KATAMBI ATOA MKWANJA MNONO KWA TIMU YA STAND UNITED IKIICHAPA MTIBWA SUGAR NA KUVUNA ALAMA 3 KAMBARAGE

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu, ametoa zawadi ya Sh,Milioni 1 kwa Timu ya Stand United (Chama la Wana), baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mchezo huo umechezwa leo Machi 17,2025 katika Uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga, na kuhudhuriwa na mashambiki pamoja na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro.

Mchezo huo ambao ni wa kufuzu kushiriki Ligi kuu ya Tanzania Bara, ambapo kipindi cha kwanza ulianza na kasi kubwa na Stand United kufanikiwa kupata penati dakika ya 8, mkwaju uliopigwa na Mchezaji Omari Ramadhani, goli ambalo lilidumu hadi dakika ya 90.
Kocha wa Timu ya Stand United Chama la wana Masoud Juma, amesema vijana wake walifuata maelekezo yake na ndiyo maana wameibuka na ushindi huo, na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kushiriki kucheza Ligi kuu ya Tanzania Bara.

“Ushindi huu umetupa Morali hivyo tutaendelea kupambana katika michezo yetu iliyosalia kwa kuhakikisha tunapata ushindi na tunawaomba wadau wa michezo pamoja na mashabiki waendelee kutu “Support”,”amesema Juma.

Kocha wa Timu ya Mtibwa Sugar Awadhi Juma, amesema mipango yao katika mchezo huo wamefeli na wenzao wametumia makosa wakapata penati na waibuka na ushindi na kwamba wanajipanga katika mchezo ujayo.

Katibu wa Mbunge Katambi Samweli Jacksoni, akizungumza kwa niaba ya Katambi, amesema Mbunge huyo ana thamini sana michezo na amekuwa akianzisha ligi mbalimbali hapa Shinyanga na amefurahishwa na Timu ya Stand United kuibuka na ushindi huo na ametoa sh.milioni moja ya kuwa pongeza na kwamba ataendelea kuwaunga mkono hadi wapande kushiriki kucheza Ligi Kuu ya Tanzania bara msimu ujao.
Kufuatia mchezo huo Timu ya Stand United inafikisha point 49 na kusalia nafasi ya 3, ambapo inakuwa na pointi sawa na Mbeya City ambayo inashika nafasi ya pili kwa tofauti ya magoli,huku Mtibwa Sugar ikisalia katika nafasi yake ya kwanza kwa point 54.

TAZAMA PICHA👇👇
Katibu wa Mbunge Katambi,Samweli Jackson akitoa pesa sh.milioni Moja kwa Timu ya Stand United baada ya kuibuka na ushindi kwa kuifunga Timu ya Mtibwa Sugar CCM Kambarage.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akiongoza hamasa katika mchezo wa Timu ya Stand United dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa CCM Kambarage.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464