GARI HII HILI LISIGEUZWE KUWA DALADALA – RC MACHA

GARI HII HILI LISIGEUZWE KUWA DALADALA – RC MACHA

Na. Paul Kasembo, SEGESE - MSALALA DC.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameutaka Uongozi wa Shule ya Sekondari ya Mwl. Nyerere iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kutogeuza matumizi ya gari la kubebea wagonjwa (school ambulance) kuwa Daladal a, kuikodisha au kuifanya kuwa ya biashara kwa namna yoyote ile kwani kufanya hivyo ni kinyume na lengo kusudiwa.

RC Macha ameyasema haya jana Machi 3, 2025 akiwa kwenye hafla ya kukabidhi gari hilo ambapo pamoja na yote amewapongeza Wazazi, Bodi ya Shule pamoja na Wadau wa Elimu kwa kushiriki katika uchangiaji wa ununuzi wa gari hilo lililogharimu zaidi ya Tzs. Milioni 26.

“Ninawasihi sana uongozi wa shule hii, walimu na wote mnaohusika kutokengeuka na kugeuza matumizi ya gari hili ambalo nimelikabidhi leo kwa kuanza kuikodisha au kuifanya kuwa daladala badala yake ikafanye kazi kulingana na malengo yaliyokusudiwa kwa ambayo ni ya kubebea wanafunzi wanaokaa bweni ambao watapata changamoto kwa namna moja au nyingine za kiafya," alisema RC Macha.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni ameupongeza uongozi wa shule, walimu na wadau wa elimu kwa jitihada za kuunga mkono Serikali katika kuboresha sekta ya elimu, lakini pia amewapongeza wanafunzi kwa matokeo mazuri kwa miaka 3 mfululizo.



Aidha Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwalimu Nyerere Mwl. Kafuru Songora ameahidi kulitunza na kulisimamia gari hilo ili litumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili lidumu kwa muda mrefu na kuwasaidia wanafunzi wanaokumbwa na changamoto za kiafya hususani kidato cha tano na sita ambao wanakaa bwenini.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Idd Kassim alisema kuwa, atashirikiana na uongozi wa Kata, Shule na wananchi katika kutatua changamoto kadhaa ambazo zililipotiwa kwenye hotuba iliyowasilishwa na kusisitizwa na baadhi ya wanafunzi ikiwemo ya upungufu wa madawati na matundu ya vyoo.


Pia Mhe. Idd aliahidi kutoa tofali 1000 kwa ajili ya kujenga Chumba Maalum cha watoto wa kike na Mashine ya kuvuta maji (motor) ambayo itakayokuwa ikitumika kuvuta maji katika kisima kinachotarajiwa kujengwa shuleni hapo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464