WANANCHI SHINYANGA WAPAGAWA NA KATAMBI UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO
-wasema Wabunge wote waliopita Shinyanga hakuna kitu,huku wakiwataja kwa majina.
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
WANANCHI wa Shinyanga,wameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa Mbunge Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu, juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kutatua changamoto zao ndani ya muda mfupi wa Ubunge wake.
Wamebainisha hayo jana kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika Kata ya mjini katikati ya mji wa Manispaa ya Shinyanga, uliohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Chama cha CCM, pamoja na Wataalamu wa Halmashauri na Taasisi za Serikali kwa ajili ya kujibu kero za wananchi.
Mmoja wa wananchi hao Sada Mohamed Salehe, amesema miaka yote Shinyanga haijawahi kupata Mbunge ambaye anajali matatizo ya wananchi na kutatua shinda zao, lakini sasa wana Mbunge ambaye ni Katambi,kuwa ndani ya muda mfupi ameubadilisha mji huo wa Shinyanga kimaendeleo.
“Wabunge wote waliopita hapa Shinyanga (aliwataja majina ambapo mimi si sawa kuwaandika sababu wengine wameshatangulia mbele ya haki)hakuna walichokifanya, lakini ameingia Katambi unayaona kabisa haya hapa maendeleo.”amesema Sada.
Amesema kulikuwa na madaraja yenye kero tangu kipindi anasoma shule ya Msingi Iwelyangula, na alikuwa akipita kwenye Mto,lakini Wabunge wote waliopita hawakuwahi kutatua matatizo hayo,lakini Utawala wa Katambi Madaraja mengi yamejengwa likiwamo la Iwelyangula, na sasa wanafunzi wanapita bila shida, tofauti na kipindi anasoma yeye alikuwa akipita mtoni.
Diwani wa Kata ya Mjini Gulaamu Mkadamu,amempongeza Katambi kwa maendeleo makubwa ambayo ameyafanya ndani ya miaka yake Minne ya Ubunge,huku akitamka maneno kwamba “Mnyonge Mnyongeni lakini haki yake mpeni”, kuwa hakuna Mbunge kama Katambi na kwamba Shinyanga imepata mtu sahihi wa kieletea maendeleo.
Katambi akizungumza kwenye mkutano huo, amesema yeye ni Mbunge wa maendeleo, huku akianza kujibu kero za wananchi likiwamo tatizo la kutowaka taa za barabarani, na kutoa maagizo kwa TARURA kwamba zifanyiwe ukarabati haraka katika barabara zao, na kuwapongeza TANROADS kwa kuanza kuzirekebisha katika barabara ambazo ni zao.
“Nikweli wananchi taa nyingi za barabarani haziwaki ni mbovu,nilishawaagiza TARURA wasifanyie pia ufuatuliaji ili kujua kama taa hizi ambazo zinanunuliwa ni bora, isije kuwa tunapigwa sababu si mara ya kwanza taa hizi kuharibika,ila nimeona baadhi ya barabara zimeanza kufungwa tena baada ya maagizo yangu, nadhani itakuwa barabara za Tanroads na nyie Tarura mzifunge kwenye barabara zenu,”amesema Katambi.
Akijibu pia suala Mikopo ya Halmashauri asilimia 10,amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri,kuwa katika utoaji wa mikopo hiyo kuwesiwe na kona kona nyingi, bali kama watu wamekidhi vigezo wapatiwe ili wanufaike nayo kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi.
“Kijana Seif Sudi ambaye umelalamika kukosa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kwa kipindi kirefu, ambayo asilimia 4 hutolewa kwa vijana,leo nakupa ofa ili kuwe mfano kwa vijana wengine wachangamkie mikopo hiyo, nenda kwa Mkurugenzi hapo meza kuu uandikishe biashara yako na kutoa taarifa zako zote na upatiwe mkopo mara moja ili upanua kiwanda chao kiitwacho Juice ya pilipili cha ushonaji viatu na utoa ajira kwa vijana,”amesema Katambi.
Ametolea maagizo pia kwenye maeneo ya vivuko vya barabara, yawekwe matatu likiwamo eneo la soko la nguzonane, ambalo wananchi walilalamikia kuwa watoto wanapata shida kuvuka kwenda shule,ili kuwaepusha na ajali.
Akizungumzia maendeleo ambayo ameyafanya kwenye Kata ya Mjini pekee, kuwa barabara nyingi ambazo zilikuwa kero ya muda mrefu zimejengwa kwa kiwango cha lami,kikiwamo na kipande cha barabara ya Empire,ujenzi wa maengesho ya magari,maeneo ya kupumzikia, pamoja na ujenzi wa soko kuu la kisasa kiwango cha ghorofa.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Peres Kamugisha, alijibu swali la mwannachi mmoja ambaye aliuliza juu ya hatima ya Machinjio ya Zamani, sababu imekuwa sehemu hatarishi,ambapo amesema kwamba mipango ya halmashauri ni kuligeuza eneo hilo kuwa Stendi ya Haice za kwenda Mwawaza kupita hospitali ya rufaa.
Mbunge Katambi bado anaendelea na ziara yake ya Kata kwa Kata katika Jimbo la Shinyanga mjini kuzungumza na Wanachama wa CCM, pamoja na kufanya mikutano ya hadhara kusikiliza kero za wananchi na kuwaeleza yale ambayo ameyatekeleza kipindi cha miaka yake Minne ya Ubunge.
TAZAMA PICHA 👇👇
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu akizungumza na wananchi wa Kata ya Mjini kwenye mkutano wa hadhara.
Diwani wa Kata ya Mjini Gulamu Mkadamu akizungumza kwenye Mkutano huo.
Mkutano wa Mbunge Katambi ukiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464