TCRA:WAANDISHI WA HABARI MSITANGAZE MATOKEO YA UCHAGUZI KABLA YA KUTOLEWA NA TUME YA UCHAGUZI
MAMLAKA ya mawasiliano Tanzania (TCRA),imewataka waandishi wa habari,kusimamia kanuni za uchaguzi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika uchaguzi mkuu 2025 wa kuchagua Madiwani,Wabunge na Rais.
Hayo yamebainishwa leo Machi 14,2025 na Meneja Kitengo cha Utangazaji Mhandisi Andrew Kisaka wakati akiwasilisha mada kwenye mkutao wa MISA-TAN na wadau SUMMIT 2025.
Amesema waandishi wa habari wakati wa kuripoti habari za uchaguzi, wanapaswa kuzingatia kanuni za uchaguzi ili kutoa taarifa zao kwa kuzingatia miongozo na kanuni zilizowekwa, pamoja na kuacha kutangazao matokeo ya uchaguzi kabla ya kutolewa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi.
“Waandishi wa habari mzingatie kanuni za uchaguzi wakati wa kutoa taarifa zenu, na msije mkatangaza matokeo kabla ya kutolewa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ili msijeleta taharuki, kama ilivyotokea Zanzibar mwaka 2010 chombo kimoja cha habari kilitangaza matokeo kabla,”amesema Mhandisi Kisaka.
Aidha,amesema pia wakati wa kuripoti habari hizo za uchaguzi au kufanya mijadala kwenye vyombo vya habari, wasingatie usawa kwa vyama vyote vya siasa na siyo kuonyesha kupendelea chama kimoja.
“Mnapaswa pia muwe na usawa kwa vyama vyote vya siasa wakati wa kuripoti habari za uchaguzi, au kuanzisha mijadala, kutoa taarifa kwa kile ambacho umekiona wala msiongeze chumvi, kuingilia faragha,au kujionyesha una mahaba na chama flani jinsi unavyo ripoti taarifa yako namna unavyotoa sauti,”ameongeza Mhandisi Kisaka.
Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Joyce Shebe,ametumia fursa hiyo kuiomba jamanii, kwamba wamuone mwanamke kama mgombea mwingine na siyo kumfanyia udhalilishaji, ili wawe na muitikio mkubwa wa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi na kuleta usawa wa kijinsia.
Mwenyekiti wa MISA-TAN Edwin Soko,amesema mijadala kama hiyo wanaijadili ili uchaguzi Mkuu ufanyike kwa Amani na utulivu,bila ya kutoa changamoto zozote.
TAZAMA PICHA👇👇
Meneja Kitengo cha Utangazaji TCRA Mhandisi Andrew Kisaka .
Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Joyce Shebe.
Mwenyekiti wa MISA-TAN Edwin Soko.