CHADEMA KANDA YA SERENGETI YAKERWA NA UTEKEJI, YAPANGA MAANDAMANO YA AMANI
Na Mwandishi Wetu,SHINYANGAPRESSBLOG
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Kanda ya Serengeti, kimelaani vikali matukio ya utekaji kuendelea hapa nchini yakihusisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, kwamba vitendo hivyo vinaleta hofu kubwa kwa jamii,huku wakimuomba Rais Samia kuunda Tume huru ya kuchunguza matukio hayo ya utekaji.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti Jacksoni Mnyawami, inayounganisha Mkoa wa Shinyanga,Mara na Simiyu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Kanda hiyo Mjini Shinyanga.
Amesema matukio ya utekaji ambayo yanaendelea hapa nchini siyo afya njema kwa taifa letu,huku akiwataja watu ambao wanadaiwa kutekwa, kuwa ni kiongozi wa hamasa wa Chadema jimbo la Tarime vijijini, Mussa Juma, na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Daniel Chonchorio, ambaye pia ni mtia nia wa Jimbo la Tarime Mjini.
“Vitendo hivi vya utekaji kuendelea hapa nchini vimeongeza hofu miongoni mwa wananchi na kuathiri hali ya usalama katika taifa letu,”amesema Mnyawami.
Katika hatua nyingine, ametangaza kuwa Chadema itaratibu maandamano ya amani ambayo yatafanyika mkoani Mara kama njia ya kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu na kuonyesha hasira dhidi ya vitendo vya utekaji.
"Tunaelekeza mkoa wa Mara kuanza kuratibu maandamano ya amani ambayo yatashirikisha viongozi wa Chadema pamoja na wanachama wa CCM, lengo letu ni kupinga utekaji unaoendelea hapa nchini hususani katika mkoa wa Mara,”amesema Mnyawami.
Aidha, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume Huru kuchunguza matukio ya utekaji, na kuongeza kwamba ripoti ya haki jinai inayobaini ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu inapaswa kutekelezwa kwa haraka.
"Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kuunda tume ya kijaji kuchunguza matukio haya ya utekaji na kuhakikisha vyombo vya ulinzi vinawajibika,”amesisitiza Mnyawami.
Pia, amewaomba wadau wa haki za binadamu na wananchi kwa ujumla kupaza sauti dhidi ya vitendo viovu vinavyoendelea hapa nchini.