KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE IMEFANYA ZIARA MKOANI SHINYANGA,KWA WAFANYABIASHARA WA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI
KAMATI ya Kudumu ya Bunge,Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, imewatembelea wafanyabiashara wanaotumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani mkoani Shinyanga. na kutoa maelekezo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara, kuendelea na tathmini ya kupanua wigo wa leseni za biashara hizo, ili wafanyabiashara hao waweze kufanya biashara katika mikoa mingine nchini.
Ziara hiyo imefanyika leo Machi 13,2025.
Wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuongeza wigo wa leseni zao ili kuwawezesha kuuza na kununua mazao katika maeneo zaidi ya mkoa wao, jambo ambalo litazidisha kuongeza ushindani wa kibiashara pamoja na kuongeza pato la taifa kwa kupanua masoko na kuongeza mapato kupitia ushuru.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Njalu Daudi, amesema kuwa leseni za sasa zinawazuia kufanya biashara katika mikoa mingine na kuomba serikali kubadilisha hali hiyo kwa kupanua wigo wa leseni.
“Hili ni ombi kwa serikali mtuongezee wigo wa leseni wa wafanyabiashara, hizi tulizonazo zinatuwekea mipaka ya kufanya biashara ndani ya mkoa husika, lakini tunahitaji kuvuka mipaka kibiashara hadi mikoani mingine, hii itasaidia kuleta ushindani,” amesema Daudi.
Mfanyabiashara mwingine, Hassan Mboje, ameeleza kuwa kuuza na kununua mazao katika mikoa mingine kutazalisha mapato zaidi kwa taifa, kwa sababu ushuru utalipwa katika kila mkoa wanapofanya biashara.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deodatus Mwanyika, alitoa maelekezo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Seleman Jafo, kuhakikisha wigo wa leseni unapanuliwa, na kutoa nafasi ya kutafuta masoko mengine kwa wafanyabiashara wa mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Natoa maelekezo kwa Waziri Seleman Jafo, waendelee na tathimini juu ya ufunguzi wa milango ya leseni kutumika hadi mikoani ,na pia katika suala zima la kutafuta masoko mengine” amesema Mwanyika.
Waziri Jafo alikubaliana na maelekezo hayo na kusema kuwa watafanyia kazi ili kuboresha utendaji wa mfumo huo wa stakabadhi ghalani.
“Maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hii ya Bunge tunayachukua na kuyafanyia kazi. ili kuboresha utendaji kazi wa mfumo wa stakabadhi ghalani” amesema Jafo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, alieleza kuwa elimu kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani imesaidia wafanyabiashara wengi kujiunga na mfumo huo, na kumekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Asangye Bangu, alieleza faida za mfumo huo, hasa katika kuhakikisha mazao yanapokuwa tayari kwa mnada, yanatenganishwa na mchanga na kusafishwa kwa kutumia chekecheo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464