SERIKALI MKOANI SHINYANGA YATAMBUA MCHANGO WA TCRS
Bugalama, MSALALA.
SERIKALI mkoani Shinyanga imeendelea kutambua michango ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali likiwemo Tanganyika Christian Refugee Service na ambalo limejikita zaidi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambapo limeendelea kuisaidia jamii katika nyanja ya afya, maji, uwezeshaji wananchi kiuchumi, elimu nk.
Pongezi na utambuzi wa mchango wake umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni katika kilele cha sherehe ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ambayo Kimkoa ilifanyika Kata ya Bugalama, Halmashauri ya Msalala ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha.
CP. Hamduni alilitaja TCRS kama moja ya Shirika ambalo limeendelea kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Mkoa na hata kuwezesha kwa namna moja au nyingine kufanikisha kwa Maadhimisho hayo huku akisema kuwa Serikali itaendelea kutambua, kuthamini na kuheshimu michanho yao.
"Ndugu Mgeni Rasmi, nitambue uwepo na mchango mkubwa kutoka kwa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali likiweko TCRS, ambao wameendelea kufanya kazi na Serikali ya Mkoa wa Shinyanga wakati wote na katika sherehe hizi wanao mchango mkubwa kwenye kufanikisha Maadhimisho haya," alisema CP. Hamduni.
Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS) lenye Makao Makuu yake Mikocheni Jijini Dar es Salaam, linafanya kazi kwa niaba ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Baraza la Makanisa la Tanzania kwa kushirikiana na Serikali likilenga kutoa misaada ya kibinadamu, kukabiliana na dharura, kutoa misaada, programu za uwezeshaji wa jamii na katika nyanja ya elimu, afya, mazingira na maendeleo ya jamii.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464