ZITTO ATOA DARASA,MJADALA TANZANIA KUNUNUA UMEME


Zitto atoa darasa,majadala Tanzania kununua umeme

Picha:Mtandao
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ametoa ufafanuzi kuhusu mjadala mkali unaoendelea kuhusu Tanzania kununua umeme kutoka Ethiopia.

Ameeleza kuwa mjadala huo umejikita zaidi kwenye umbali wa usafirishaji badala ya kuelewa mfumo wa biashara ya umeme katika sekta ndogo ya nishati.

Kwa mujibu wa Zitto, biashara ya umeme wa mipakani (cross-border power trade) haifanyi kazi kwa kusafirisha umeme moja kwa moja kutoka nchi moja hadi nyingine. Badala yake, umeme huwekwa katika gridi ya pamoja (power pool), kisha nchi zinafanya biashara kati ya zile zenye ziada (surplus countries) na zile zenye upungufu (deficit countries).

Ametoa mfano kwamba Tanzania ikinunua 100MW kutoka Ethiopia, umeme huo unaingia kwenye gridi ya Kenya, kisha Kenya inatoa kiasi hicho cha umeme kwa Tanzania kupitia kituo cha nguvu cha mpakani. Kwa maana hiyo, Tanzania inapokea 100MW Namanga, mkoa wa Arusha, badala ya kuusafirisha moja kwa moja kutoka Ethiopia.

Amesema Tanzania ikizalisha umeme kutoka Rufiji na inausafirisha hadi Arusha kupitia gridi moja ya taifa. Hata hivyo, katika safari hiyo, kuna upotevu wa umeme (transmission loss) unaoweza kufikia asilimia 15-20. Kinyume chake, umeme unaoingia kutoka Namanga haupotezi kiasi kikubwa cha nishati kwa sababu unaingia moja kwa moja kwenye matumizi, ukipitia vituo vya kupoza umeme (power stations) kutoka 400kV hadi 66kV, kisha 33kV na hatimaye 11kV kwa matumizi ya majumbani.

Zitto amefananisha mfumo huo na utaratibu wa kutuma pesa kwa M-Pesa, ambapo pesa hazihamishwi kutoka wakala mmoja hadi mwingine, bali mtumiaji huchukua pesa kutoka kwa wakala anayetoa huduma. Hali ni kama hiyo kwa umeme, ambapo Tanzania inachukua umeme mpakani bila kusafirisha kutoka Ethiopia moja kwa moja.

SOMA HAPA ZAIDI CHANZO NIPASHE

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464