RCC SHINYANGA YARIDHIA JIMBO LA SOLWA KUGAWANYWA KUWA NA MAJIMBO MAWILI YA UCHAGUZI
KIKAO cha Kamati cha Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC)kimeridhia mapendekezo ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)kuligawa jimbo la Solwa,kuwa na Majimbo Mawili ya Uchaguzi ambayo ni Solwa na Itwangi.
RC Macha.
Kikao hicho kimefanyika leo Machi 15,2025 kikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Macha, amesema baada ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)kutoa vigezo na mapendekezo kwa ajili ya kuligawa jimbo la Solwa,kwamba kunapaswa kufuatwa taratibu zingine za vikao,kikiwamo Kikao cha Baraza cha Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,kikao cha Kamati cha ushauri wilaya ya Shinyanga DCC, na kikao cha Mkoa RCC, ili kujadili vigezo na kupitisha mapendezo hayo ya kuligawa jimbo hilo.
Amesema vikao viwili tayari vilishafanyika,ambavyo ni Baraza la Madiwani na Kikao cha Kamati ya Ushauri wilaya ya Shinyanga (DCC), na leo wamekaa Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) na wamepitia vigezo vyote vilivyotolewa na Tume ya uchaguzi kwa ajili ya kuligawa jimbo la Solwa, kwamba vigezo vyote wamekidhi na wameridhia jimbo hilo ligawanywe.
“Kigezo cha kwanza kilichotolewa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi, ni Idadi ya watu, ambapo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi mwaka 2022, jimbo hilo la Solwa lina watu 468,611, lakini takwimu za mwaka huu 2025, kuna ongezeko la watu na kufika 503,167, na ukigawanya jimbo la Solwa litakuwa na watu 309,821, na Itwangi 193,346, hivyo tumekidhi vigezo,”amesema Macha.
“Kigezo kingine ni ukubwa wa eneo,ambapo Jimbo la Solwa lina ukubwa Kilomita za Mraba 4,212, eneo ambalo ni kubwa sana, na linakigezo jimbo hili kugawanywa,”ameongeza Macha.
Aidha, amesema jimbo hilo litakapogawanywa, Jimbo la Solwa litakuwa na Kata 12, na Itwangi Kata 14, na kwamba kukiwa na Wabunge wawili kutasaidia wananchi kuwa karibu na Wabunge wao, huku akimpongeza Mbuge wa Solwa Ahmed Salum, kwa kuchapa kazi ya kuwahudumia wananchi wote wa jimbo hilo licha ya ukubwa wake.
“Jimbo hilo la Solwa limekidhi vigezo vyote vya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi kuligawa, kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi, Solwa yenyewe na Itwangi,kikao cha RCC kimeridhia Jimbo hili ligawanywe,”amesema Macha.
Amesema baada ya kikao hicho cha RCC kupitisha na kuridhia mapendekezo ya kuligawa Jimbo hilo la Solwa, taarifa zake zitapelekwa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)kabla ya tarehe 26 Machi mwaka huu ili mchakato wa kuligawa uanze.
Aidha,Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),ilitangaza baadhi ya majimbo kugawanywa, na kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi, likiwamo Jimbo la Solwa wilayani Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464