Wasira afungua ofisi ya CCM Chibe iliyojengwa na Katambi
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira,amefungua ofisi ya CCM Kata ya Chibe, ambayo imejengwa na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi.
Ameifungua Ofisi hiyo leo Machi 26,2025, ikiwa ni miongoni mwa Ofisi mbili za Chama, ikiwamo ya Ibadakuli,ambazo zimejengwa na Mbunge Katambi,ambaye ni Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu.
Amempongeza Mbunge Katambi kwa ujenzi wa Ofisi hizo za Chama,na kueleza kwamba ofisi hizo zitumike kusikiliza maoni ya wanachama pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
"Chama chetu cha CCM ni daraja kati ya serikali na wananchi,na ofisi hii itumike kufanya vikao vya Chama,pamoja na kupanga mikutano ya kueleza wananchi juu ya utekelezaji wa ahadi ambazo zimetekelezwa na serikali chini ya Rais Samia,"amesema Wasira.
Mjumbe wa NEC Richard Kasesela, amempongeza Mbunge Katambi,kwa ujenzi wa Ofisi hizo,kwamba amekiheshimisha Chama.
Katibu wa CCM Kata ya Chibe Kasokila Kameja, akisoma taarifa ya ujenzi wa Ofisi hiyo ya Chama, amesema ulianza Mei mwaka jana na kukamilika Novemba mwaka huo.
Amesema Ofisi hiyo imejengwa na Mbunge Katambi, kwa gharama ya sh.milioni 51.7, na kwamba imekuwa mkombozi kwao kwa shughuli za kichama.