MAAFISA UGANI NA WADAU WA ZAO LA PAMBA KISHAPU WAMETAKIWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA KUONGEZA UZALISHAJI NA TIJA

Maafisa Ugani na Wadau wa Zao la Pamba Wametakiwa Kushiriki Kikamilifu Katika Kuongeza Uzalishaji na Tija

Na Ofisi ya Habari,KISHAPU

MKUU wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amewataka maafisa ugani na wadau wa zao la pamba kushirikiana kikamilifu ili kuongeza uzalishaji na tija katika sekta hiyo.

 Amesema kuwa wadau hawa ni muhimu katika maendeleo ya zao la pamba na si wakulima pekee.
Mhe. Masindi amebainisha hayo jana, Machi 11, 2025, wakati wa kikao kilichohusisha maafisa ugani, watendaji wa vijiji, AMCOS, na wadau wa zao la pamba. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa SHIRECU kwa ajili ya kutathmini maendeleo ya zao la pamba kwa wakulima.

Akizungumza na wadau hao, Mhe. Masindi alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa pamoja katika kutatua changamoto, kero, na matatizo yanayowakumba wakulima. Aliwaambia maafisa ugani, AMCOS, Bodi ya Pamba, na watendaji wa vijiji kuwa ni muhimu kuwa kitu kimoja wanapokutana na changamoto ili kumsaidia mkulima na kuhakikisha pamba inapatikana kwa wingi. Hii itasaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa katika uzalishaji wa zao la pamba.
“Mnapotoka hapa, hakikisheni mnakutana kama timu – Afisa Ugani, Bodi ya Pamba, mtu wa BBT, Afisa Ushirika, na mtendaji wa kata. Tafuteni suluhisho la kufanikisha uzalishaji wa pamba mwezi wa Tano. Binadamu ameumbwa kutatua changamoto za wengine, na hakuna mtu aliyeumbwa kuleta matatizo. Hivyo, mkawe kitu kimoja katika kutatua changamoto za wakulima kwa kushirikiana,” alisema Mhe. Masindi.

Kwa upande mwingine, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mwl. Sigthbeth Rwezahula, alisisitiza kuwa maafisa ugani na wadau wa pamba wanapaswa kushirikiana ili kuleta tija katika uzalishaji wa zao la pamba katika mwaka 2025 na miaka ijayo.

Aidha, Mhe. Masindi alitoa agizo la kupiga marufuku maafisa ugani kujihusisha na shughuli nyingine zisizo za kilimo, kwani zinapelekea kushindwa kuwahudumia wakulima wa pamba ipasavyo. Alitaka wataalamu wa kilimo wilayani Kishapu kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu taratibu bora za kilimo cha pamba ili kuongeza tija na uzalishaji, na kuacha kilimo cha mazoea.

Wakulima wa pamba wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwajali na kutoa msaada katika sekta ya kilimo cha pamba, licha ya changamoto ndogondogo kama vile upungufu wa sumu ya kupulizia wadudu kutokufika kwa wakati.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464