Mjumbe wa kituo cha taarifa na maarifa Kata ya Kishapu Monica Machiya katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 7,2025 katika hospitali ya Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.
Na Sumai Salum-Kishapu
Kituo cha taarifa na maarifa Kata ya Kishapu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP kimeadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kuwatembelea wanawake wajawazito na wanawake wenye watoto katika hospitali ya Wilaya ya Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Akizungumza Machi 7 wakati akikabidhi zawadi mbalimbali za sabuni na kutoa pongezi kwa wanawake hao Mwenyekiti wa Kituo cha taarifa na marifa Modesta Machiya amesema wameona vema kuwatembelea wanawake wenzao ili kukumbushana kuendelea kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwenye jamii zao.
"Wanawake wenzangu nawapongeza sana kwa kuwa Mungu ametuamini Sisi kutuweka kuwa kielelezo kikuu na chanzo cha mambo mema duniani, hivyo tukumbuke kesho tunapofikia kilele cha siku ya wanawake kidunia tunaowajibu wa kuendelea kupata sauti popote pale ukatili unapokea ama kuona kiashiria chochote cha ukatili",ameongeza Modesta.
Amesema ukatili kwa sasa unaendelea kupungua kutokana na juhudi mbalimbali za serikali,taasisi zisizokuwa za kiserikali na jamii kwa ujumla hivyo kila mwanamke anatakiwa kuchukia ukatili kwa nguvu zote.
Aidha,Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dr. Ester Nyange amewapongeza kituo cha taarifa na maarifa kwa moyo wa kuwakumbuka wahitaji hasa kundi la kina mama linalokabiliwa na adha ikiwemo kukataliwa na waume wanaowapa mimba kupelekea kukosa mahitaji muhimu.
"Tunaamini mnaendelea kutoa elimu ya ukatili na wanawake watambue nafasi zao katika familia hasa ya kujiongezea kipato ili wawasaidie watoto wao wa kike kwenye mahitaji,hii itasaidia kuondokana na mimba na ndoa za utotoni kwani ni hatarishi hasa kwenye afya ya uzazi na kupelekea uzazi pingamizi", amesema Dr. Nyange
Amesema kumekuwepo na baadhi ya wasichana chini ya miaka kumi na nane(18) kupata ujauzito na hatimaye kutokuwa na ujasiri wa kurudi kwendelea na elimu baada ya kujifungua hivyo siku hii itawakumbusha wanawake na kuwapa ujasiri wa kukabiliana na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.
Kwa upande wake muuguzi kiongozi wodi ya wazazi Hilda Ebunka amewapongeza kituo cha taarifa na maarifa kwa kuwatembelea wanawake na kuwapa zawadi na kuwasihi iwe ni tabia ya mara kwa mara na si siku ya wanawake pekee kwani wako wanaohitaji msaada wanatoka kwenye kaya duni.
Bi Ester Joramu mkazi wa Mhunze Wilayani humo ameiomba serikali na mashirika yanayotekeleza miradi ya ukatili kuendelea kutoa elimu zaidi huku akitoa wito kwa wanaume kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini wake zao.
Aidha Khadija Khamis mkazi wa Kiloleli ameshukuru kwa zawadi alizopewa na kuwaomba kutembelea na vituo vya afya na zahanati zilizoko vijijini ili kuwasaidia wanawake wengine kwa kuwajengea uelewa na ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kilele chake ni Machi 8, 2025, yenye kaulimbiu "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” yatakayofanyika Jijini Arusha huku mgeni rasmi akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hasan.
Ester Joram (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa Kata ya Kishapu Modesta Machiya(kushoto) katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 7,2025 katika hospitali ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.
Muuguzi kiongozi wodi ya wazazi Hilda Ebunka akizungumzia changamoto wanazokutana nazo pindi wanapomzalisha mjauzito mwenye umri chini ya miaka kumi na nane(18) kwa wawakilishi kutoka kituo cha taarifa na maarifa kwa kushirikiana na TGNP walipokuwa wakiadhimisha Siku ya wanawake duniani Machi 7,2025
Mjumbe wa kituo cha taarifa na maarifa Kata ya Kishapu Mahembo Ngassa (suti ya bluu) akikabidhi zawadi kwa mzazi katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 7,2025 katika hospitali ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.
Kaimu Mganga Mfawidhi hospitali ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Dr. Ester Nyange akizungumza na wawakilishi kutoka kituo cha taarifa na maarifa kata ya Kishapu kwa kushirikiana na TGNP katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani Machi 7,2025 walipoenda kutoa zawadi na kuzungumza na wanawake wodi ya wajawazito na wazazi
Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Kishapu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Modesta Machiya akielezea madhara yatokanayo na ukatili mbalimbali kwenye wodi ya wazazi hospitali ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Wilayani humo machi 7,2025 katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani wakishirikiana na TGNP
Afisa muuguzi kitengo cha watoto wenye changamoto za kiafya chini ya mwezi mmoja hospitali ya Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mwanaisha Kassim kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani machi 7,2025 wakati kituo cha taarifa na maarifa kata ya Kishapu wakitoa zawadi kwa wazazi na wajawazito