*Ni katika muendelezo wa kampeni ya elimu kwa umma kuhusu Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri Chalinze mkoani Pwani
*NSSF yaahidi kufikisha elimu ya hifadhi skimu kwa wananchi wengi zaidi
Na MWANDISHI WETU, PWANI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewaongoza mamia ya wananchi wa Chalinze mkoani Pwani, katika muendelezo wa elimu kwa umma kuhusu Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri yenye jina la kampeni "NSSF STAA WA MCHEZO".
Akizungumza na wananchi waliojiajiri, mwishoni mwa wiki iliyofanyika Chalinze mkoani Pwani, Mhe. Ridhiwani ameipongeza NSSF kwa kuja na skimu hiyo ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi waliojiajiri ili kunufaika na mafao ya muda mfupi yakiwemo ya matibabu na mafao ya muda mrefu ambayo ni uzeeni.
Mhe. Ridhiwani amewataka wananchi waendelee kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye. "Unapojiunga na skimu hii pale unapougua utanufaika na matibabu, ukipata ulemavu utanufaika na mafao ya ulemavu, ukiwa mzee utanufaika na mafao ya uzeeni hivyo ni muhimu kila mwananchi kuchangamkia fursa hii, kwa kujiweka akiba," amesema Mhe. Ridhiwani.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maoni na miongozo yake ambapo kupitia Serikali ya awamu ya sita, wananchi waliojiajiri wanajiwekea akiba NSSF na kunufaika na mafao na huduma nyingine.
"Mpango ulioletwa na NSSF ni kwa ajili ya leo na kesho yako, kwani itafika siku nguvu ya kufanyakazi zitapungua na hapo ndipo NSSF itachukua nafasi ya kuwa Staa wa Mchezo kwa kulipa mafao ya pensheni ya uzee na matibabu," amesema Mhe. Ridhiwani.
Amesema NSSF imeweka utaratibu nzuri wa kujiunga na kuchangia kidogo kidogo kwa siku buku buku, hivyo amewataka wananchi kuendelea kujiunga na kuchangia ili kunufaika na mafao pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na Mfuko.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Omary Mziya, amesema hifadhi skimu inawahusu wananchi waliojiajiri katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kuwa inaenda kufungua milango kwa wananchi kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF yakiwemo na matibabu.
Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Mhe. Hassan Mwinyikondo ameipongeza NSSF kwa kuja na skimu hiyo ambayo itakuwa mkombozi wa wananchi waliojiajiri.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga amemewahakikishia wananchi wa Chalinze na Bagamoyo kuwa mpango huo ni mkombozi kwa wananchi hususani watakapoishiwa nguvu ya kufanyakazi, kwani watapata mafao kutoka NSSF.