WAZIRI RIDHIWANI AZINDUA BODI YA WADHAMINI YA NSSF

  

*Aitaka Bodi kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, sera na miongozo inayotolewa na Serikali

*Mkurugenzi Mkuu asema NSSF inatekeleza azma ya Rais Dkt. Samia ya kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa kuwafikia wananchi waliojiajiri

Na MWANDISHI WETU,

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amezindua Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuitaka kutekeleza majukumu yake kwa kusimamia sheria, sera, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali.

Uzinduzi wa Bodi hiyo umefanyika tarehe 14 Machi, 2025 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba, Naibu Katibu Mkuu TALGWU, Bw. Wandiba Ngocho, Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Mwakilishi kutoka Msajili wa Hazina pamoja na Menejimenti ya NSSF.

Mhe. Ridhiwani ameitaka Bodi hiyo pia kusimamia Mpango Mkakakati wa Mfuko unaozingatia uboreshaji wa huduma ya wanachama, michango, uwekezaji na kulipa mafao.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema Mfuko unaendelea kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii na kuwafikia wananchi waliojiajiri waweze kujiunga na kuchangia ili wanufaike na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko.

Amesema suala la wananchi kujiunga na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii ni ajenda ya dunia na ya nchi na kuwa lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama, ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe, Rais Dkt. Samia imelipa umuhimu wa pekee.

“Ninakushukuru Mhe. Waziri kwa namna ambavyo umelishikia bango jambo hili, umeshirikiana na sisi tangu tuanze kampeni yetu ya “NSSF Staa wa Mchezo” kuhakikisha waliojisajili wanakuwa sehemu ya hifadhi ya jamii kama ambavyo nchi zilizoendelea zimewasajili wananchi waliojiajiri,” amesema Bw. Mshomba.

Amesema kwa mujibu wa malengo 17 ya dunia, kila lengo linazungumzia masuala ya hifadhi ya jamii kwa sababu ili uweze kuondoa umasikini ni hatua ya kwanza wananchi wa taifa husika wawe ni wanufaika wa hifadhi ya jamii, kwa sababu kupitia hifadhi ya jamii mwanachama au mwananchi wanakuwa na uhakika wa maisha na kipato.

“Ndio maana tunasema “NSSF Staa wa Mchezo” kwa maana ukiwa mwanachama wa NSSF wewe utang’aa, utakuwa Staa katika maisha yako yote, wakati ukiwa na nguvu za kufanya kazi na hata baada ya kumaliza kufanya kazi, NSSF inakuwa Staa wa kukupa pensheni ya uzee, hivyo nawaomba wananchi waendelee kujiunga na kuchangia ili wawe Mastaa wa Mchezo wa sasa na baadaye.

Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Mary Maganga amewataka wajumbe wa Bodi kusimamia Mfuko kwa uadilifu na kuzingatia maslahi mapana ya wanachama.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Bi. Mwamini Malemi ameahidi kufanya kazi kwa kufuata sheria, sera na miongozo iliyopo kwa mustakabali wa Mfuko.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464