KLABU YA WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA “SPC” IMEFANYA MKUTANO MKUU WA WANACHAMA,MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KUSHIRIKIANA NA VYOMBO VYA HABARI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC),imefanya mkutano mkuu wa wanachama,huku Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga,ikiahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari,pamoja na kutoa mafunzo namna ya kuandika habari za kimahakama kwa kuzingatia sheria na miongozo.
Mkutano huo umefanyika leo Aprili 5,2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,huku Mgeni Rasmi akiwa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Ntuli Mwakahesya, akimwakilisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Frank Mahimbali.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru, akisoma taarifa ya Klabu hiyo kwa Mgeni Rasmi, amesema mkutano huo ni takwa la kikatiba kwa ajili ya kujadiliana maendeleo ya ustawi wa klabu.
“Katika mkutano wetu huu mkuu, leo tutajadili taarifa za maendeleo ya klabu yetu na kufanya maamuzi ya kimuundo, kwa utawala kwa kupitisha bodi ya klabu ili tuendane na mabadiliko ili kuwa na klabu ya ustahimilivu wa kusonga mbele zaidi,”amesema Kakuru.
Aidha,ameiomba Mahakama kuu Kanda ya Shinyanga, kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari, pamoja na kutoa mafunzo maalumu namna ya kuandika habari za Kimahakama, na hata kufanya ziara kutembelea miradi ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo, ili kuwajulisha umma hatua za ujenzi wa miradi hiyo.
“Ndugu Mgeni Rasmi kuna mabadiliko mengi ya kisheria yameendelea kutokea juu ya uendeshaji wa kesi mbalimbali na changamoto kubwa iliyopo, na sehemu kubwa ya waandishi si wabobezi wa kuandika habari za mahakama licha ya kufundishwa vyuoni bali tunahitaji kukumbashana zaidi,hivyo tunaomba Mahakama mtupatie mafunzo namna ya kuandika habari za kimahakama,amesema Kakuru na kuongeza.
“Tunaomba pia mafunzo yatakayosaidia waandishi wa habari katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu, kwa kuzingatia sheria sababu kuna baadhi ya sheria zimetungwa kwa ajili ya uchaguzi hivyo ni vyema waandishi wa habari wakazifahamu ili wanapotekeleza majukumu yao watekeleze kwa weledi.”
Katika hatua nyingine, amesema Klabu hiyo imepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka 2020-2025, pamoja na kuendesha kampeni ya ukatili yenye thamani ya sh.milioni 66.7, kufungua ofisi ya waandishi wa habari katika Ofisi ya wilaya ya Kahama,kuongeza Idadi ya wanachama,kuongeza rasilimali ardhi,kujenga mahusiano na wadau ngazi ya mkoa na taifa.
Mafanikio mengine ni kuendesha miradi ya kihabari kwa radio jamii,kuwajengea uwezo wanachama kupitia mafunzo na ziara,kuunda sera mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya ndani ya taasisi na kuaminiwa na shirika la maendeleo ya sweeden (SIDA), kama Klabu Imara na bora.
“Mfanikio haya yamechagizwa na ushirikiano mzuri kutoka kwa Sekretarieti ya SPC,Kamati Tendaji na wanachama wote,”amesema Kakuru.
Mgeni Rasmi katika Mkutano huo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Ntuli Mwakahesya,ameipongeza Klabu hiyo kwa mkutano wao pamoja na kuwa miongoni mwa Klabu bora hapa nchini,huku akiahidi Mahakama hiyo itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari.
Ameahidi pia Mahakama hiyo,itaandaa mafunzo kwa waandishi wa habari namna ya kuandika habari za Kimahakama,huku wakiwasihi wanahabari wawe wanafika Mahakamani na kuandika habari na kuhabarisha umma.
Amewasihi pia waandishi wa habari, kwamba katika kipindi cha uchaguzi mkuu,wanapokuwa wakiandika habari zao wazingatie maadili na miiko ya taaluma yao,pamoja na kuhakiki vyanzo vya taarifa kutoka kwenye vyanzo sahihi ambavyo vina aminika.
Katika mkutano huo shukrani zimetolewa kwa TASAF,Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Kiwanda cha Jambo, SHIDEFA,BENKI ya CRDB,Life Water,Ruwasa,Shuwasa, Manispaa ya Kahama,Jeshi la Zimamoto na uokoaji,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, huku wakiwakaribisha wadau wengine kushirikiana na Klabu hiyo.
TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru akizungumza kwenye mkutano huo.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Patrick Mabula akizungumza kwenye mkutano huo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Ntuli Mwakahesya akizungumza kwenye mkutano huo.
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka TASAF Christopher Kidanka akizungumza kwenye mkutano huo.
Viongozi wakiwa Meza Kuu.
Wanachama wa SPC wakiwa kwenye mkutano.
Picha ya pamoja.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464